1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Pompeo kuelezea mipango ya Trump kuhusu Iran

Sekione Kitojo
29 Aprili 2018

Mwanadiplomasia  wa  ngazi ya juu  wa  Marekani Mike Pompeo alitarajiwa  kukutana  na  viongozi wa  Saudi Arabia  na  Israel leo Jumapili (29.04.2018) kutafuta mshikamano wa pamoja  katika upinzani dhidi  ya  Iran.

Saudi-Arabein Riad Mike Pompeo trifft Außenminister Adel Al-Jubeir in Riyadh
Picha: Reuters/Saudi Press Agency

Waziri wa mambo  ya  kigeni wa  Marekani Mike Pompeo aliwasili mjini  Riyadh jana  Jumamosi  muda  mfupi  baada  ya  waasi wanaoungwa mkono  na  Iran  wa  Kihuthi  nchini  Yemen  kufyatua kombora  katika  mpaka na  nchi  hiyo  ya  Kifalme.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Mike Pompeo akipokewa na waziri wa mambo ya kigeni wa Saudia Adel Al-JubeirPicha: Reuters/Saudi Press Agency

Pompeo alikula chakula  cha  usiku  pamoja  na mrithi wa  kiti  cha Ufalme  nchini  Saudi  Arabia Mohammed Bin Salman , na  leo Jumapili  alitarajiwa  kukutana  na   baba yake  mfalme Salman.

Baadaye  alitarajiwa   kusafiri  kwenda  Jerusalem  kukutana  na waziri  mkuu  wa  Israel Benjamin  Netanyahu na  kisha  atakwenda Amman  Jordan, akikamilisha  mazungumzo  ya  mwishoni  mwa  juma na  baadhi  ya  mahasimu  wakubwa wa  Iran  katika  kanda  hiyo.

Trump kusitisha  makubaliano  na  Iran

Trump  anatarajiwa  hapo Mei 12 ama  kurejesha  vikwazo  vya kinyuklia  dhidi  ya  Tehran, na kuuweka  mkataba  huo wa  mwaka 2015  katika  mashaka, ambapo  mataifa  mengi  yenye  nguvu duniani  yanauona  kuwa  muhimu  katika  kuizuwia  Tehran  kupata silaha  za  kinyuklia.

Lakini  trump  na  washirika  wa  nchi  hiyo  katika  mashariki  ya  kati wanadai  makubaliano  hayo  yaliyoidhinishwa  na  mtangulizi  wa Trump , Barack Obama , ni  dhaifu  mno  na  yanahitaji  kubadilishwa na  makubaliano  mengine  zaidi  ya  kudumu na  kusaidiwa  na udhibiti  katika  mpango  wa  Iran  wa  makombora.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Mike Pompeo akiwasili Saudi ArabiaPicha: Reuters/Saudi Press Agency

Pompeo  alianza  ziara yake  ya  kwanza  ya  kidiplomasia  ndani  ya masaa  mawili  baada  ya  kuapishwa  siku  ya  Alhamis  na  siku  ya Ijumaa , baada  ya  mazungumzo  na  washirika  wa  NATO  mjini Brussels, alionekana  kudokeza  kwamba  Trump  anapanga kusitisha  makubaliano  hayo.

Mwandishi : Sekione  Kitojo / afpe

Mhriri: Yusra Buwayhid