1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Pompeo kuhojiwa na Maseneta Marekani

Isaac Gamba
25 Julai 2018

Maseneta wa bunge la Marekani wanatarajia kumuhoji  waziri wa mambo ya nje   Mike Pompeo kama kuna jambo ambalo Trump  alimuahidi ama kumueleza rais Vladimir Putin  wakati walipokutana katika mkutano wao wa kilele.

Mike Pompeo
Picha: picture-alliance/AP Photo/M. J. Terrill

Maseneta nchini Marekani wanaoonekana kuumizwa  na tabia ya hivi karibuni ya bilionea huyo wa chama cha Republican watahitaji kupata majibu  hii leo  Jumatano  kutoka kwa waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo wakati atakapowasilisha  taarifa ya utendaji wake wa kazi  akiwa ni mwanadiplomasia wa ngazi ya juu wa nchi hiyo ikiwa ni kipindi kifupi tangu ashike wadgifa huo.

Hayo yanajiri wakati wa bunge nchini Marekani wakiwa na shauku ya kufahamu kutoka kwa Pompeo juu ya mkutano  muhimu wa kilele  kati ya rais Donald Trump na kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong  Un uliofanyika  Juni 12 nchini Singapore.

Shauku ya wabunge hao  imeongezeka na kuonekana kuwa suala la haraka na muhimu zaidi baada ya mkutano wa Helsinki, hususani kikao cha pamoja kati ya viongozi hao wawili na waandishi wa habari ambapo  Trump alionekana  kwa wabunge wa chama chake cha Republican na wale wa Democrat kusaliti masilahi ya Marekani  na kuonekana  kukubaliana na   Putin.

" Mkutano na waandishi wa habari wa Helsinki ulikuwa ni siku mbaya kwa nchi yetu na kila mtu anajua hilo" amesikika seneta Bob Corker,  mwenyekiti wa   kamati  inayohusiana na mahusiano ya kimataifa wa chama cha Republican  ambaye  pia  amekuwa akimkosoa mara kwa mara rais Donald Trump alipozungumza na waandshi wa habari.

 

Mkutano wa  Helsinki kupewa kipaumbele

Rais Donald Trump wa MarekaniPicha: picture-alliance/Captital Pictures/R. Sachs

Suala la Urusi linatarajiwa kuchukua uzito  wakati  wa kikao kati ya Mike Pompeo na  kamati ya bunge la Congress.

Hata hivyo Corker ameweka bayana kuwa kamati yake pamoja na mambo mengine itamuhoji pia waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo juu ya safari yake ya hivi karibuni nchini Korea Kaskazini,  kauli ya rais Donald Trump dhidi ya  NATO, Suala la ushirikiano wa pamoja katika masuala ya ulinzi, na msimamo wa Trump kuhusiana na viwango vipya vya kodi ambao sasa unaonekana kutaka kusababisha vita vya kibiashara.Pompeo amesema ataeleza mbele ya kamati hiyo juu ya masuala mengi likiwemo suala la uhusiano  kati ya Marekani  na Urusi na zaidi mkutano wa kilele kati ya Trump na rais  Vladimir Putin wa Urusi.

Kikao hicho cha ndani kati ya Trump na Putin kimekosolewa na wabunge nchini Marekani  lakini Pompeo amesisitiza kwamba mkutano huo umuhimu wake kwa dunia utaonekana hapo baadaye wakati historia itakapoandikwa.

Ikulu ya Marekani White House imetangaza kwamba rais wa Urusi Vladimir Putin amealikwa nchini Marekani kwa ajili ya mkutano mwingine baadaye mwaka huu mnamo wakati  bunge la Congress likionekana kukerwa  na yale yaliyojiri katika ziara ya Trump mjini Helsink hivi karibuni hasa alipoonekana  kukubaliana  na kauli ya Putin kukanusha kuingilia uchaguzi mkuu wa Marekani wa mwaka 2016 hatua iliyoonekana kupingana na uchunguzi wa mashirika ya kijasusi ya Marekani  uliohitimisha  Urusi iliingilia uchaguzi huo.

Kauli hiyo ya Trump mjini Helsinki ilisababisha mjadala  mkubwa nchini Marekani kiasi ya kiongozi huyo  kusema aliteleza ulimi  na baaday kufafanua  kuwa ana amini  Urusi iliingilia uchaguzi huo.

Mwandishi: Isaac Gamba/ AFPE

Mhariri :Bruce Amani