Pompeo kutangaza mkakati wa Marekani kuhusu Iran
21 Mei 2018Pompeo atawasilisha muelekeo wa kidiplomasia utakaolenga kutafuta mkataba mpya wa nyuklia na Iran katika hotuba atakayoitoa katika taasisi ya Heritage mjini Washington. Hotuba ya Pompeo inakuja wiki mbili baada ya Rais Donald Trump wa Marekani kuiondoa nchi yake kutoka kwa mkataba kati ya Iran na nchi za Magharibi ulioafikiwa mwaka 2015 na kuuwekea upya vikwazo utawala wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Tehran.
Wizara ya mambo ya nje ya Marekani imesema Pompeo aliwasiliana na mawaziri wa mambo ya nje wa Ujerumani, Ufaransa na Uingereza, kabla hotuba yake.
Hapo jana, Marekani ilisema inatumai itatumia masilahi ya pamoja yaliyojitokeza miongoni mwa mataifa washirika barani Ulaya katika miezi ya hivi karibuni kuendeleza jitihada zake za kuuboresha mkataba wa nyuklia na Iran, mpango wa utengenezaji makombora na jukumu lake katika usuluhishi wa mizozo ya kikanda.
Iran ilisema juhudi za Umoja wa Ulaya kuuokoa mkataba wa nyuklia hazitoshi, huku ikilalamika kuhusu kampuni za mataifa ya Ulaya kusitisha uwekezaji wake katika Jamhuri hiyo ya Kiislamu.
Rais wa Iran, Hassan Rouhani, alisema njama ya Marekani kuitenga nchi yake kwa kujitoa kutoka kwa mkataba wa kimataifa wa nyuklia haijafua dafu licha ya juhudi kubwa zilizofanywa. "Tumefaulu kuwashinda maadui zetu wanaopiga vita sera yetu ya nje. Tulishinda njama kubwa ya kwanza. Utawala wa Marekani ulitaka kuitenga Iran lakini wakapata matokeo kinyume kabisa na matarajio yao. Hatukuiruhusu Marekani kutimiza lengo lake na njama yao iligonga mwamba."
Iran kushiriki mkutano wa Vienna
Iran ilisema jana itajiunga na wanadiplomasia kutoka Ujerumani, Uingereza, Ufaransa, China na Urusi katika mkutano unaopangwa kufanyika mjini Vienna, Austria, Ijumaa wiki hii kujadili hatua za kuchukua baada ya uamuzi wa Rais Trump kuindoa Marekani kutoka kwa makubaliano ya nyuklia na Iran alioutangaza Mei 8.
Iran pia ilisema Marekani itashiriki katika mkutano wa mjini Vienna wa tume ya pamoja iliyoundwa na mataifa sita yenye nguvu duniani, Iran na Umoja wa Ulaya, kwa nia ya kuyatafutia ufumbuzi malalamiko yaliyojitokeza kuhusiana na utekelezaji wa mkataba huo.
Gazeti la Ujerumani la Welt am Sonntag lilimnukulu afisa wa ngazi ya juu wa Umoja wa Ulaya akisema mazungumzo yanaendelea kuhusu uwezekano wa mkataba mpya kati ya Iran na dola kuu za dunia utakaojumuisha misingi ya mkataba wa mwaka 2015, lakini utakaokuwa na vipengee vingine vipya vitakavyoongezwa ili kuiridhisha Marekani.
Chanzo hicho kilisema vipengee hivyo huenda vikaushughulikia wasiwasi wa Marekani kuhusu mpango wa makombora wa Iran na hatua ya utawala wa nchi hiyo kuyafadhili makundi yaliyojihami na silaha Masahriki ya Kati. Mkataba huo mpya huenda ukajumuisha msaada wa kifedha kwa Iran.
Mwandishi: Josephat Charo/Reuters/dpa/AP
Mhariri: Mohammed Khelef
Mwandishi:Josephat Charo/dpae/rtre/
Mhariri:Mohammed Khelef