Pompeo: Tuna msimamo mkali kwa Urusi
2 Julai 2020Haya yanakuja wakati ambapo uiongozi wa Trump umeghadhabishwa na ripoti zilizochapishwa kwenye magazeti kwamba kitengo cha ujasusi Marekani kinaamini kuwa Urusi iliwalipa wanamgambo wa Taliban kwa ajili ya kuwauwa wanajeshi wa Marekani.
Rais Donald Trump kupitia kwa katibu wa ikulu ya White House Kayleigh McEnany amekanusha kwamba hakutaarifiwa kuhusiana na suala hilo.
"Kulikuwa hakuna makubaliano ya pamoja miongoni katika kitengo cha ujasusi na isitoshe, miongoni mwa hao maafisa wa ujasusi kulikuwa na wengine wanaopinga na kwa sababu kulikuwa hakuna thibitisho, taarifa hiyo haikumfikia rais," alisema Kayleigh.
Trump hupenda kupuuza taarifa za kijasusi
Lakini mshauri wa zamani wa Trump katika masuala ya usalama wa kitaifa John Bolton ambaye kwa sasa anakinadi kitabu alichokiandika na kinachomkosoa rais huyo wa Marekani pakubwa amesema iwapo ni kweli kwamba Urusi imewalipa wanamgambo wa Taliban kwa ajili ya kuwauwa wanajeshi wa Marekani basi hilo ni jambo linalostahili kuangaziwa kwa umuhimu mkubwa mno.
Bolton vile vile amesema rais Trump ni mtu anayependa kupuuza kila anapopewa taarifa za kijasusi kuhusiana na matukio.
"Tatizo la Donald Trump si kwamba hapendi kupokea kutaarifiwa, ukweli ni kwamba hapendi kuambiwa ukweli. Mikutano ya kijasusi haitoi taarifa kama inavyostahili, tulijaribu kufikiria mbinu za kubadilisha jambo hilo lakini juhudi zetu hazikuzaa matunda. Si ati kwamba idara ya ujasusi inafeli ila rais hatilii maanani taarifa anazopewa kama vile watangulizi wake walivyokuwa wakifanya," alisema Bolton.
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo amesema "si jambo jipya" kwamba Urusi inaiendea kinyume Marekani huko Afghanistan kwani kulingana na Pompeo wamekuwa wakiuza silaha ndogo ndogo nchini humo na kuyaweka maisha ya Wamarekani hatarini, ila ametetea jinsi serikali ilivyojibu madai hayo.
Marekani bado inaweza kumualika Putin
Licha ya yote hayo, Pompeo hajauondoa uwezekano wa kumualika Rais Putin Marekani. Mwezi uliopita Trump alitafakari kumualika kiongozi huyo wa Urusi katika mkutano wa kilele wa nchi saba zilizoendelea kiviwanda G7.
Utawala wa Trump umeendelea kusema kwamba bado haiko wazi iwapo kweli Urusi iliwalipa wanamgambo wa Taliban kwa ajili ya kuwashambulia wanajeshi wa Marekani. Madai hayo yalifichuliwa na vyombo vya habari vya Marekani mnamo mwishoni mwa wiki na ni jambo ambalo kwa sasa linamla kichwa Trump katika mwaka wa uchaguzi mkuu nchini humo.
Urusi imeyakanusha madai hayo dhidi yake.