PORT HARCOURT: Mhandisi wa Lebanon auwawa
23 Februari 2007Watu wasiojulikana wamempiga risasi na kumuua muhandisi raia wa Lebanon katika mji wa mafuta wa Port Harcourt nchini Nigeria.
Mauaji hayo ni tukio la hivi punde la mashambulio dhidi ya wafanyakazi wa kigeni nchini Nigeria, ambako mashambulio ya mwanamgambo yamepunguza mauzo ya mafuta katika mataifa ya kigeni kwa asilimia 20 na kuwalazimu maelfu ya wafanyakazi wa kigeni kuihama nchi hiyo.
Utekaji nyara na mashambulio dhidi ya wafanyakazi wa kampuni za mafuta yamekuwa matukio ya karibu kila wiki katika eneo la Niger Delta, ambalo linaongoza katika utoaji wa mafuta barani Afrika.
Wafanyakazi wanane kati ya tisa kutoka mataifa ya kigeni wanazuiliwa na makundi mbalimbali yenye silaha katika eneo Niger Delta, baada ya mmoja wao raia wa Lebanon kuponyoka juzi Jumatano.
Wakati haya yakiarifiwa, wizara ya mashauri ya kigeni ya Italia imetangaza leo kwamba mafundi wawili raia wa Italia wametekwa nyara wakati wa ufyatulianaji wa risasi mjini Port Harcout kusini mwa Nigeria.