Presseschau: Maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani
5 Oktoba 2017Mhariri wa gazeti la Die Welt anasema ikiwa mawasiliano hayatadumishwa ndani ya Uhispania jimbo mojawapo tajiri katikati mwa barani Ulaya litakuwamo katika hatari ya vita vya wenyewe kwa wenyewe. Mhariri anatilia maanani mfululizo wa matukio ya kusikitisha ukiwa unaelendelea, muflisi wa Ugiriki,ushindi wa makundi yenye itikadi kali za mrengo wa kulia, mgogoro wa wakimbizi na kura ya maoni juu ya Uingereza kujindoa Umoja wa Ulaya (Brexit).
Naye mhariri wa Die Volksstimme ameandika pia juu ya mgogoro wa Catalonia anasema kiogozi wa jimbo la Catalonia, Carles Puigdemont ameitisha kura ya maoni mapema mno na hivyo kusababisha uchokozi wa hali ya juu kabisa. Kwa bahati mbaya Waziri Mkuu Mariano Rajoy amefanya pupa na ameingia katika mtego kwa kuwapelaka polisi waliotembeza virungu kwa waandamanaji. Katikati ya Ulaya katika karne hii ya 21, kushindwa kwa viongozi wachache kuchukua hatua sahihi, kunaweza kusababisha maafa makubwa.
Nini kitafanyike baada ya maafa ya Las Vegas kutokea
Gazeti la Aachener Zeitung linasema ikiiwa wendawazimu huo hautokomeshwa kwa sheria kali, hakuna kitakachobadilika nchini Marekani. Lakini uwezekano wa kubadilisha sheria ya umiliki wa bunduki ni nunge kabisa kwenye bunge la Marekani linalodhibitiwa na wajumbe wa chama cha Republican. Na kutokana na uwepo wa rais Trump anaetaka kuwaruhusu watu kuwa na silaha kote nchini Marekani ina maana uwezekano huo kwa sasa haupo.
Kuhusu mkutano mkuu wa chama cha kihafidhina cha Uingereza
Gazeti la Stuttgarter Zeitung juu ya mkutano mkuu wa chama cha kihafidhina nchini Uingereza. Mhariri wa gazeti hilo ameandika kwamba mkutano huo uliofungwa kwa hotuba ya Waziri Mkuu Theresa May ulikuwa wa maafa. Mhariri wa gazeti hilo la Stuttgarter Zeitung anaeleza kwamba kwanza waziri wake wa mambo ya nje Boris Johnson kwa ujeuri alimpa changamoto kwa kuupinga mkakati wake juu Uingereza kujiondoa kutoka kwenye Umoja wa Ulaya. Bibi May pia alipaswa kwa muda wa siku tatu kusikiliza jinsi mawaziri wake pamoja wajumbe wengine walivyokuwa wanalumbana juu ya nchi yao kujiondoa Umoja wa Ulaya (Brexit) kana kwamba kadhia hizo hazikutosha, sauti yake ilikauka wakati alipoihitaji zaidi kuwapa sauti hiyo wale waliosahauliwa katika jamii ya Waingereza.
Mwandishi: Zainab Aziz/ Deutschen Zeitungen
Mhariri: Iddi Ssessanga