1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Presseschau: Maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani

27 Septemba 2018

Wahariri katika safu zao za maoni leo wanazungumzia juu ya mvutano kati ya Umoja wa Ulaya na Marekani kuhusu Iran na pia Msikiti unaotarajiwa kufunguliwa na rais wa Uturuki katika jiji la Cologne.

Türkei Präsident Erdogan
Picha: Getty Images/AFP/A. Weiss

Süddeutsche Zeitung

Maoni ya mhariri wa gazeti la Süddeutsche juu ya hali ya maendeleo ya kiuchumi katika Ujerumani mashariki tangu kuungana tena kwa Ujerumani mbili zaidi ya miaka 25 iliyopita. Mhariri wa gazeti hilo anazungumzia juu ya ripoti iliyochapishwa na serikali kuhusu muungano huo.

Ukuta uliondolewa miaka mingi iliyopita kati ya Ujerumani mashariki na ya magharibi. Ni kweli kwamba Ujerumani mashariki imepiga hatua katika maendeleo ya kiuchumi lakini bado haijaweza kufikia kiwango cha Ujerumani magharibi. Tofauti katika viwango vya maisha inadhihirika pia katika kauli za watu. Aghalabu watu wa upande wa mashariki huwaita wale wa upande mwingine kuwa ni "wamagharibi”. Hisia za ghadhabu zinastawi mashariki mwa Ujerumani dhidi ya taasisi za kidemokrasia.

Mhariri wa gazeti hilo la Süddeutsche anasema kinachokosekana, mashariki mwa Ujerumani ni ari ya kushiriki katika ujenzi wa jamii kwa njia chanya lakini pia upande wa magharibi unapaswa kuwa tayari kuendesha mdahalo kwa njia ya usawa. Mhariri anasema katika enzi hizi za sera ya dunia utandawazi, mawimbi ya wahamiaji na siasa za kizalendo inawapasa viongozi wa vyama vyote vya kisiasa wauunge mkono upande wa mashariki kwa sauti kubwa!

Westfalen-Blatt

Gazeti la Westfalen-Blatt linatoa maoni juu ya mvutano kati ya Umoja wa Ulaya na Marekani kuhusu mkataba wa nyuklia uliofikiwa na Iran. Mhariri wa gazeti hilo anaeleza kwamba kila mtu angependelea, wakati wote kuuona Umoja wa Ulaya ukisimama kwa uthabiti, kama unavyofanya sasa. Yeyote yule, ikiwa pamoja na rais wa Marekani Donald Trump anayejiondoa  kwenye mikataba ya kulinda mazingira na ya biashara huru, au anayejindoa kwenye taratibu zinazoleta maendeleo ya dunia, huyo kamwe asitegemee kuungwa mkono na yeyote na hasa ikiwa anajiondoa kwenye mkataba uliofikiwa na Iran juu ya kuzuia kuundwa silaha za nyuklia.

Kölner Stadt-Anzeiger

Mhariri wa gazeti la Kölner Stadt-Anzeiger juu ya mvutano kati ya Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan na meya wa jiji la Cologne juu ya msikiti anaotarajiwa kuufungua katika mji huo siku ya Jumamosi. Mhariri huyo anatilia maanani kwamba meya wa mji huo amekataa kushiriki kwenye sherehe za ufunguzi kwa sababu ya kuwepo kwa rais Erdogan.

Mhariri huyo anasema Uturuki inatoa masharti kwa Meya wa mji wa Cologne juu ya ufunguzi wa msikiti huo. Meya Henrietta Rekers amepinga kwa sababu rais wa Uturuki ndiye atayekaufungua. Mhariri anahoji hadi meya Rekers kufika mbali kiasi hicho  kwa nini jambo hilo haliachiliwi mbali! ili kufikia mwafaka kwanza.

Mwandishi: Zainab Aziz/Deutsche Zeitungen

Mhariri: Mohammed Khelef

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW