1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Putin aamuru vikosi vya kujilinda viwe kwenye tahadhari

27 Februari 2022

Rais wa Urusi, Vladmir Putin ameamuru kwamba vikosi vya kuzuia mashambulizi vya nchi hiyo viwekwe katika hali ya tahadhari. Putin amesema amemtaka waziri wa ulinzi na mkuu wa majeshi kuviandaa vikosi hivyo.

Lage in der Ukraine nach Beginn des russischen Angriffs
Picha: Alisa Yakubovych//EPA-EFE

Putin ametaja vikosi vya kuzuia mashambulizi kwa silaha za kujikinga, lakini hakutaja waziwasi vikosi vyake vya nyuklia.

"Viongozi wakuu wa nchi zinazoiongoza Jumuia ya Kujihami ya NATO wanatoa kauli za uchochezi dhidi ya nchi yetu, hivyo naamuru vikosi hivyo katika jeshi la Urusi viwekwe katika utaratibu maalum wa tahadhari," alisema Putin wakati akihutubia kupitia televisheni.

Hatua hiyo ameichukua kutokana na vikwazo kadhaa ambavyo vimewekwa dhidi ya Urusi baada ya nchi hiyo kuivamia Ukraine, ambavyo vinaonekana kuuyumbisha uchumi wa Urusi.

Kwa upande wake Ukraine imesema kwamba mji wa Kharkiv bado uko mikononi mwa vikosi vyake. Taarifa hii ni kutokana na shambulizi la mapema lililofanywa na vikosi vya Urusi.

Rais wa Urusi, Vladimir PutinPicha: Sergei Guneyev/AFP

Mji huo na maeneo yanayouzunguka, ikiwemo bomba la gesi ulilengwa na mashambulizi ya usiku kucha kwa bunduki na magari ya kijeshi ya Urusi yaliripotiwa kuonekana majira ya Jumapili asubuhi.

Hata hivyo, baadae Gavana wa Kharkiv, Oleh Sinegubov aliandika katika mtandao wa Telegram kwamba mji huo uki chini ya udhibiti kamili wa Ukraine, baada ya kudai kuwa vikosi vya Ukraine vimewasambaratisha wanajeshi wa Urusi wakati wa operesheni.

Soma zaidi: Urusi: Mazungumzo na Ukraine hayatositisha mashambulizi

Wakati huo huo, Ukraine imekubali kushiriki mazungumzo ya amani na Urusi, ambapo wajumbe wa pande zote mbili wamepanga kukutana katika eneo la mpaka kati ya Belarus na Ukraine. Hayo ni kwa mujibu wa taarifa ya ofisi ya Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky.

Taarifa inasema hakuna masharti yoyote yaliyowekwa katika mazungumzo hayo ya mpakani. Awali Zelensky alikataa kukutana na wajumbe wa Urusi katika eneo lililoanishwa na serikali ya Urusi kwa madai kwamba taifa hilo kwa sehemu fulani lilipanga uvamizi wake nchini Belarus.

Huku hayo yakijiri, Rais Zelensky amefungua mashtaka dhidi ya Urusi katika mahakama ya juu kabisa ya Umoja wa Mataifa ya mjini The Hague kufuatia mgogoro baina ya mataifa hayo mawili.

Rais wa Ukraine, Volodymyr ZelenskyPicha: Ukrainian Presidential Office/ABACA/picture alliance

Hata hivyo, haijawekwa wazi sababu za kesi hiyo kufikishwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki, ICJ. Maafisa wa mahakama hawajaweza kupatikana mara moja kuelezea hatua hiyo.

Lakini katika ukurasa wake wa Twitter, Zelensky ameandika kwamba Urusi lazima iwajibike kwa kuendesha kile alichokiita mauwaji ya halaiki na kuhalalisha ukandamizaji na kuomba uamuzi wa haraka wa kuiamuru Urusi kusitisha shughuli zake za kijeshi.

Scholz aapa kuongeza matumizi ya ulinzi

Kansela wa Ujerumani, Olaf Scholz amesema uamuzi wa kuruhusu upelekwaji wa silaha Ukraine ilikuwa njia pekee ya kukabiliana na uchokozi wa Putin. Akilihutubia Bunge la Ujerumani katika kikao maalum kuhusu uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, Scholz amesema ni Putin ndiyo amechagua vita hivyo, sio watu wa Urusi, hivyo lazima waone wazi kuwa hivyo ni vita vya Putin.

Scholz pia ametangaza mpango wa kuongeza matumizi kwa jeshi la Ujerumani akiahidi euro bilioni 100 kwa bajeti ya 2022 kwa majeshi yake na kurudia ahadi yake ya kufikia asilimia 2 ya matumizi ya Pato la Taifa katika ulinzi sambamba na matakwa ya NATO.

"Katika kuishambulia Ukraine, Putin hataki tu kuitokomeza nchi hiyo kutoka kwenye ramani ya dunia, bali anavurunga muundo wa usalama wa Ulaya ambao tumekuwa nao tangu Helsinki," alisisitiza Scholz wakati akiwahutubia wabunge.

Kansela wa Ujerumani, Olaf ScholzPicha: FABRIZIO BENSCH/REUTERS

Ama kwa upande mwingine wizara ya uchukuzi na miundombinu ya kidijitali ya Ujerumani imetangaza kwamba ndege za Urusi zimepigwa marufuku katika anga ya nchi hiyo kuanzia saa tisa alasiri Jumapili.

Waziri anayehusika na wizara hiyo, Volker Wissing ametangaza uamuzi huo baada ya nchi nyingine kadhaa kufunga anga zake kwa ajili ya ndege za Urusi.

Ujerumani imeungana na nchi za Ulaya Mashariki ambazo ni wanachama wa Umoja wa Ulaya pamoja na Uingereza katika kuichukua hatua hiyo. Nchi nyingine kadhaa zilizoungana na Ujerumani Jumapili ni pamoja na Italia, Iceland na Uholanzi.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, Liz Truss ameonya kuwa vita vya Ukraine havitamalizika haraka. Truss amekiambia kituo cha televisheni cha Sky News kwamba wanahitaji kujiandaa kwa safari ndefu, kwani inaweza kuchukua miaka kadhaa kwa sababu wanachojua ni kwamba Urusi ina vikosi imara.

Amesema licha ya vikwazo vikali sana dhidi ya Urusi, itachukua muda kwa uchumi wake kuathirika. Aidha, Truss ameonya kwamba Rais Putin anaweza kutumia njia mbaya zaidi na matokeo ya vita yanaweza kuwa "mwanzo wa mwisho" wa utawala wake nchini Urusi.

Bennett azungumza na Putin

Waziri Mkuu wa Israel, Naftali Bennett amezungumza na Rais Putin kwa njia ya simu kuhusu mzozo wa Ukraine. Taarifa iliyotolewa na ofisi ya waziri mkuu wa Israel imeeleza kuwa viongozi hao wawili wamejadiliana kuhusu hali inayoendelea kati ya Urusi na Ukraine.

Ikulu ya Urusi, Kremlin imesema kuwa Putin amemueleza Bennett kuhusu operesheni maalum ya kijeshi kuilinda Donbas. Putin pia amewashutumu maafisa wa Ukraine kwa kupoteza fursa ya kufanya mazungumzo baada ya Urusi kuivamia Ukraine.

Waziri Mkuu wa Israel, Naftali BennettPicha: Nir Elias/dpa/picture alliance

Taarifa hiyo imeeleza kuwa Putin pia amesema ujumbe wa Urusi uko kwenye mji wa Gomel, Belarus na uko tayari kwa mazungumzo na wawakilishi wa Ukraine ambao bado hawajaitumia fursa hiyo.

Ikulu ya Urusi imesema Bennett kwa upande wake amependekeza Israel iwe mpatanishi katika mazungumo baina ya Urusi na Ukraine kwa lengo la kusitisha uhasama. Taarifa kutoka shirika la Habari la Israel, Khan ilieleza kwamba Rais Zelensky aliiomba Israel kuwa mpatanishi baada ya Urusi kuivamia Ukraine. Benett na Zelensky walizungumza siku ya Ijumaa.

Zaidi ya wakimbizi 360,000 wamekimbia Ukraine

Kamnishna mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi, UNHCR amesema idadi ya wakimbizi wanaokimbia vita nchini Ukraine imezidi watu 368,000. Katika taarifa yake aliyoitoa kupitia mtandao wa Twitter, amesema idadi hiyo inazidi kuongezeka.

Aidha, msemaji wa UNHCR, Chris Meizer amesema kwa makadirio ya Jumamosi zaidi ya watu 150,000 wamekimbilia Poland, na mataifa mengine ikiwemo Hungary na Romania. Poland imesema hadi Jumapili mchana zaidi ya wakimbizi 156,000 wameingia katika mipaka ya taifa hilo katika kipindi cha saa 48 pekee. Shirika hilo limesema wakimbizi wengi ni wanawake na watoto.

Wakimbizi wa Ukraine wakiwa katika mpaka wa PolandPicha: Czarek Sokolowski/AP Photo/picture alliance

Naye kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis ameendelea kutoa wito wa kumalizwa kwa mapigano Ukraine ambayo yameingia siku yake ya nne, baada ya Urusi kuivamia nchi hiyo. Akizungumza na waumini katika uwanja wa Mtakatifu Peter, Papa Francis ametoa wito wa kufunguliwa haraka kwa njia za kibinaadamu kwa ajili ya raia wanaokimbia mashambulizi.

"Ninawafikiria wazee, wale wote wanaotafuta hifadhi kwa sasa, akina mama wanaokimbia na watoto wao. Hawa ni ndugu zetu ambao ni muhimu kufungua haraka njia za kibinaadamu na wanapaswa tuwapokee," alisisitiza Papa Francis.

Ulaya inahitaji kujiandaa kuwapokea mamilioni ya wakimbizi

Kamishna wa masuala ya ndani wa Umoja wa Ulaya, Ylva, Johansson amesema umoja huo unahitaji kujiandaa kwa ajili ya mamilioni ya wakimbizi kutoka Ukraine ambao wanaingia kwenye umoja huo.

Akizungumza Jumapili na waandishi habari mjini Brussels, Johansson amesema wanahitaji kujiandaa na kuongeza kusema kuwa anaunga mkono kuanzishwa kwa agizo la ulinzi wa muda la Umoja wa Ulaya ili kutoa makaazi kwa watu wanaoingia kwenye Umoja wa Ulaya.

Mnamo mwaka 2001, agizo hilo lilikuwa jibu kwa Umoja wa Ulaya kutokana na kufurika kwa watu wengi waliohamishwa wakati wa vita vya Yugoslavia na Kosovo. Chini ya sheria zake, watu waliohamishwa kutoka nchi zisizo wanachama wa Umoja wa Ulaya walipewa ulinzi wa haraka na wa muda.

(AFP, DPA, AP, Reuters, DW https://bit.ly/3HppmjG)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW