1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Putin aapishwa kuwa Rais kwa muhula wa nne

7 Mei 2018

Vladimir Putin ameapishwa kwa muhula wa nne leo kama rais wa Urusi katika sherehe iliyofanyika katika ikulu ya Kremlin mjini Moscow. Putin alishinda muhula wa nne katika uchaguzi wa mwezi Machi.

Russland Putin Amtseinführung
Picha: Reuters/Sputnik/A. Nikolskyi

Rais huyo alipata asilimia 77 ya kura zote zilizopigwa.

Putin amekuwa rais wa Urusi kwa miaka 18 na alijiuzulu mwaka 2008 kutokana na ukomo wa muhula ila aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu na akaendelea kuiongoza nchi hiyo hadi aliporudi tena kama rais mwaka 2012.

Katika hotuba ya kuapishwa kwake Putin amesema, "nachukulia kwamba ni jukumu langu na lengo langu la maisha kuifanyia Urusi chochote, sasa na katika siku za usoni, kama rais nitafanya kadri ya uwezo wangu kuongeza nguvu na ustawi wa Urusi."

Putin lakini amekaa kimya kuhusiana na suala la kuondoka madarakani licha ya kuwa ni jambo ambalo hawezi kuliepuka kutokana na kuwa katiba ya Urusi haimruhusu kuwania tena urais baada ya mwaka 2024 muhula wake wa nne utakapokwisha.

Putin anapinga kuzorota kwa uchumi wa Urusi

Amekuwa na wakati mgumu kuufufua uchumi wa Urusi baada ya Moscow kuwekewa vikwazo na mataifa ya Magharibi kufuatia hatua yake ya kuipokonya Ukraine eneo la Crimea na zaidi ya hayo kuanguka kwa bei za mafuta duniani mwaka 2016 kulichangia pia kulemaa kwa uchumi wa Urusi. Lakini yeye mwenyewe anakanusha kuzorota kwa uchumi.

Rais Vladimir Putin kabla kuapishwa kwakePicha: Reuters/S. Bobylyov

"La muhimu zaidi ni kwamba, katika miaka yote hii nchi imekuwa ikistawi," alisema Putin, "haijapambana tu na matatizo yaliyoibuka bali ilisonga mbele na kuongeza uwezo wake," aliongeza rais huyo.

Kuapishwa kwake lakini hakujawafurahisha wengi. Inaripotiwa kwamba watu wake wa karibu wameandaa sherehe ndogo tu ambayo haitajumuisha karamu ya kifahari ya chakula ili umma usiwe na picha mbaya kuhusu serikali yake.

Upinzani nchini Urusi haujaridhishwa na hatua ya rais huyo kuingia madarakani kwa muhula wa nne kwani kumekuwa na maandamano yaliyopelekea kamatakamata. Serikali za nchi za Magharibi na wanaharakati wa haki za kibinadamu wameelezea kughadhabishwa kwao na hatua hiyo.

Polisi waliwapiga na kuwaburuza barabarani waandamanaji

Huyu hapa mmoja wa waandamanaji hao.

Polisi wa Urusi wakikabiliana na waandamanaji wanaompinga PutinPicha: Getty Images/AFP/M. Zmeyev

"Sifurahii kabisa kwamba Putin anaingia katika muhula wake wa nne au sijui ni wa tano. Nafikiri anashikilia nafasi hii kinyume cha sheria," alisema mwandamanaji huyo.

Mjini Moscow, Saint Petersburg na miji mingine kadhaa ya Urusi, hakukuwa na idhini ya maandamano hayo kufanyika na polisi walitumia nguvu kuwatimua waandamanaji ambapo waliwapiga na kuwaburuza barabarani

Mwandishi: Jacob Safari/AFPE/DPAE

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman