1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUrusi

Putin ahutubia tamasha la Red Square baada ya ushindi mnono

Hawa Bihoga
19 Machi 2024

Rais Vladimir Putin amepongeza "kurejea" kwa Urusi kwa maeneo yaliotwaliwa na Ukraine, baada ya kushinda uchaguzi ulioshutumiwa kuwa sio halali na mataifa ya Magharibi.

Picha ya putin ikipamba tamasha la Red Square
Picha ya Rais Putin na bendera ya Urusi zikipamba tamasha la Red Square mjini MoscowPicha: Maxim Shemetov/REUTERS

Jasusi huyo wa zamani alishinda kwa asilimia 87 ya kura katika uchaguzi uliofanyika kwa siku tatu, ikijumuisha upigaji kura katika maeneo ya Ukraine yanayodhibitiwa na vikosi vya Urusi.

Moscow imeonesha kwamba uchaguzi wa rais uliofanyika mwishoni mwa juma umethibitisha kuwa Warusi wanamuunga mkono Putin, zaidi ya miaka miwili ya vita ndani ya Ukraine.

Ushindi huo wa Putin unatarajiwa kuimarisha zaidi uongozi wake nchini Urusi, ambapo upinzani hauna nafasi tena ukikabiliwa na ukandamizaji unaoshika kasi.

Akiwa katika mamlaka tangu siku ya mwisho ya mwaka 1999, kwa sasa yuko mbioni kuwa kiongozi wa Urusi alietawala ndani ya kipindi cha zaidi ya karne mbili.

"Bega kwa bega, tunasonga mbele, na hii itatufanya kuwa na nguvu zaidi... Idumu milele Urusi." Putin aliuambia umati wa watu waliohudhuria tamasha la muziki la Red Square, kuadhimisha miaka 10 tangu Urusi kutwaa rasi ya Crimea kutoka Ukraine.

Soma pia:Putin aweka rekodi kwenye matokeo ya uchaguzi Urusi

Alijigamba kwa kiunganishi kipya cha reli katika maeneo ya Ukraine yaliotekwa na vikosi vya Urusi, akisema maeneo hayo yalikuwa "yametangaza shauku yake ya kurejea kwenye familia yao ya asili."

Kwenye tamasha hilo alionekana pamoja na wagombea watatu walioshindana nae kwenye sanduku la kura baada ya kuwakaribisha kwenye mkutano wa Kremlin ambao wote walimpongeza.

Hata hivyo wapinzani wake wengi wa kweli wamekufa, wakiwa gerezani, ama uhamishoni, huku uchaguzi huo unafanyika mwezi mmoja baada ya mkosoaji mkubwa wa Putin Alexei Navalny kufariki gerezani.

Uhamasishaji kwa Warusi kupiga kura

Mamalaka nchini Urusi zilitolea mwito wapiga kura kujitokeza na kushiriki kikamilifu katika uchaguzi huo ikiwa kama wajibu wa kizalendo.

"Vladimir ndiye msingi wa nchi yetu," Viktoria, mfanyakazi wa teknolijia ya mawasiliano mwenye miaka 23 katika kampuni ya serikali, alisema alipokuwa akielekea kwenye tamasha la Red Square.

Mpiga kura akipiga kura katika uchaguzi uliomalizika JumapiliPicha: Alexander Polegenko/TASS/dpa/picture alliance

Kwa upande wake Elena ambae ni mchumi mwenye umri wa miaka 64, alisema hakushangazwa na matokeo hayo, "kwa sababu nadhani kwa raia yeyote ambae anaheshimu nchi yetu, alimpigia kura Putin."

Soma pia:Putin: Urusi haitarudishwa nyuma

Zoezi hilo la upigaji kura kwa siku tatu pia lilifanyika katika maeneo ya Ukraine ambayo yanadhibitiwa na wanajeshi wa Urusi, kulikuwa na kura zilizoharibika kufuatia mashambulizi ya mabomu ya Ukraine.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky, ambaye amemshutumu rais Putin kwa kile alichokisema kwa kutaka "kutawala milele," amelihimiza Bunge la Marekani kupitisha kwa haraka msaada wa kijeshi wa dola bilioni 60.

Salamu za pongezi kutoka kwa washirika wa Putin zamiminika

Ikulu ya Kremlin ilisema kuwa rais Putin alifanya mazungumzo ya simu na washirika wake wa zamani wa muungano wa Kisovieti wa Asia ya kati ambao ni Belarus na Azerbaijan pamoja na rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan, ambao walimpongeza kwa matokeo ya uchaguzi, huku wakijitolea kufanya upatanishi kati ya Moscow na Kyiv.

Vyombo vya habari vya Urusi pia vimeripoti kuwa Putin pia alipokea pongezi kutoka kwa washirika wake wa karibu ambao ni China Korea Kaskazini, Venezuela na Myanmar.

Putin ashinda uchaguzi wa rais

01:34

This browser does not support the video element.

Soma pia:Ushindi wa Rais Putin wazua hisia mseto duniani

Hata hivyo matokeo hayo yaliompa ushindi wa kishindo Putin yalikabiliwa na kauli kali kutoka kwa mataifa ya Magharibi-tofauti na chaguzi nne zilizopita ambazo Putin alishinda tangu 2000.

"Uchaguzi huu umetokana na ukandamizaji na vitisho," Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrel alisema.

Uingereza pia imeshutumu uchaguzi huo na kusema kuwa haukuwa wa huru na haki.

"Putin anawaondoa wapinzani wake wa kisiasa, anadhibiti vyombo vya habari, na kisha kujitawaza mshindi. Hii sio demokrasia," waziri wa mambo ya nje wa Uingereza David Cameron alisema katika taarifa yake.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW