1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Putin:Tutafakari namna ya kumaliza janga la vita vya Ukraine

Hawa Bihoga
22 Novemba 2023

Rais wa Urusi Vladimir Putin amewaambia viongozi wa G20 Jumatano kwamba ni muhimu kufikiria namna ya kumaliza "janga" la vita vya Ukraine, katika moja ya matamshi ya kutuliza tangu kuzuka kwa vita hivyo mwaka liopita.

Urusi | Mkutano wa Video wa G20 | Putin
Rais wa Urusi Vladmir Putin akihudhuria mkutano wa kilele wa G20 kwa njia ya vidio.Picha: Mikhail Klimentyev/AFP/Getty Images

 

Akiwahutubia viongozi wa mataifa yalioendelea na yanayoinukia kiuchumi ya G20 kwa mara ya kwanza tangu kuzuka kwa vita, rais Putin  alisema baadhi ya viongozi walisema katika hotuba zao kwamba wameshangazwa na "uchokozi" unaoendelea wa Urusi huko Ukraine.

"Hatua za kijeshi mara zote ni janga" Putin aliuambia mkutano wa G20 ulioitishwa na Waziri Mkuu wa India Narendra Modi.

"Na bila shaka, tunapaswa kufikiria jinsi ya kukomesha janga hili," Putin alisema na kuongeza kwamba mara zote taifa lake halijawahi kukataa mazungumzo ya amani na Ukraine.

Matamshi hayo, ingawa yamekusudiwa kuzifikia jumuia za kimataifa, ni mojawapo ya maneno tulivu zaidi ya Putin kuhusu vita hivyo katika miezi kadhaa na yanatofautiana na kauli zake kali baadhi ya wakati ambazo zinazungumzia kushindwa na kiburi cha Marekani.

Soma pia:Putin asema Urusi tayari ishapeleka nafaka za bila malipo Afrika 

Vita nchini Ukraine vilivyozuka manamo Februari 2022 vimeua na kujeruhi maelfu ya watu, huku wengine mamilioni wakiyahama makazi yao na kuharibu maeneo ya kusini na mashariki mwa nchi hiyo.

Putin alitumia neno "vita" kuelezea mzozo huo badala ya neno la sasa la Kremlin la "operesheni maalum ya kijeshi".

Rais wa Urusi Vladmir Putin, kulia, na Naibu Waziri Mkuu wa Urusi, Alexey Overchuk, wa kili kulia, wakihudhuria mkutano maalumu wa G20 kwa njia ya vidio, wakati Waziri Mkuu wa India Narendra Modi akionekana kwenye skrini mjini Moscow, Urusi, Jumatano, Novemba, 22, 2023.Picha: Mikhail Klimentyev/AP Photo/picture alliance

"Ninaelewa kuwa vita hivi, na vifo vya watu, vinastua," Putin alisema, kabla ya kuibua hoja za Urusi kwa Ukraine iliwatesa watu wa Mashariki mwa Ukraine.

Mzozo wa mashariki mwa Ukraine ulianza mwaka 2014 baada ya rais anayeiunga mkono Urusi kuondolewa katika kile kilichoitwa Mapinduzi ya Maidan, na Urusi kuitwaa Rasi ya Crimea, huku vikosi vya kujitenga vinavyoungwa mkono na Urusi vikipambana na wanajeshi wa Ukraine.

Takriban watu 14,000 waliuawa katika mzozo huo kati ya 2014 na mwishoni  mwa 2021, kulingana na Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa, ikiwa ni pamoja na raia 3,106.

Soma pia: Urusi yazidisha mashambulizi katika mji wa Ukraine wa Avdiivka

"Na mauaji ya raia wa Palestina katika Ukanda wa Gaza leo, hayashtui?" Putin alihoji. Pia alisema ilikuwa inashtusha sana kwamba madaktari mjini Gaza walilaazimika kufanya upasuaji kwa watoto bila ganzi.

Washirika wa Ukraine waonesha mshikamono zaidi

Nchi za Magharibi na Ukraine zimeapa mara kwa mara kuishinda Urusi katika vita na kuviondoa vikosi vya Urusi katika ardhi ya Ukraine, ingawa kushindwa kwa ukraine katika kujibu mashambulizi katika mwaka huu, kumeibua wasiwasi kwa washirika wake nchi za Magharibi kuhusu mafanikio katika uwanja wa vita.

Pamoja na Crimea, ambayo Moscow iliitwa kimabavu mwaka 2014, Urusi inadhibiti karibu asilimia 17.5 ya eneo la Ukreine, hii ni kwa mujibu wa makadirio ya Kituo cha Belfer katika chuo cha  Kennedy Harvard. Putin anasema eneo hilo sasa ni sehemu ya Urusi.

Wakati Rais wa Marekani Joe Biden na viongozi wengine wa nchi za Magharibi wameahidi kuiunga mkono Ukraine, kuna ongezeko la mgawanyiko kuhusu misaada kwa Ukraine katika Bunge la Marekani.

Rais Joe Biden wa Marekani, kulia, akiwa na mwenzake wa Ukraine, Volodymyr Zelenskiy mjini Washington, Desemba 21, 2022. Marekani na washirika wake wameahidi kuendelea kuisaidia Ukraine kuushinda uvamizi wa Urusi.Picha: Kevin Lamarque/REUTERS

Baadhi ya wabunge wa Marekani wanatoa kipaumbele cha misaada kwa Israel hata kama maafisa wa ulinzi wa Marekani wanasisitiza kuwa Washington inaweza kusaidia washirika wote wawili kwa wakati mmoja.

Soma pia: Viongozi wa G20 waliogawika waelekea India kwa mkutano wa kilele

Ukraine imeapa kupambana katika uwanja wa vita hadi askari jeshi wa mwisho kuondoka katika ardhi yake, licha ya baadhi ya raia wa Ukraine kutoa mikakati tofauti

Putin hakuhudhuria mkutano uliopita wa mataifa hayo ya G20 mjini New Delh na huko Nusa Dua,Indonesia na badala yake aliwakilishwa na waziri wa mambo ya nje Sergei Lavrov.

Rais Putin alihutubia mkutano wa G20 mnamo 2020 na 2021 akiwa mjini Moscow, wakati mkutano wake wa mwisho kuhudhuria bayana ilikuwa 2019 huko Osaka Japan.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW