Putin aitishia Kyiv kwa makombora mapya ya masafa ya kati
29 Novemba 2024Kombora la kisasa la Oreshnik lilitumika kwa mara ya kwanza wiki iliyopita dhidi ya mji wa viwanda wa Dnipro nchini Ukraine, hatua ambayo ilionekana kama kuongezeka kwa hatari ya mzozo huo.
Putin amesema Kremlin kwa sasa inachagua maeneo ya mashambulizi zaidi, na yanaweza kujumuisha majengo ya kijeshi, kampuni za ulinzi, au vituo vya maamuzi jijini Kyiv.
Soma pia: Putin aonya kuwa vita vya Ukraine vinachukua mkondo wa kidunia
Akizungumzia shambulio la wiki iliyopita dhidi ya Dnipro, alisema walilazimika kufanya majaribio hayo chini ya mazingira ya vita kutokana na mashambulizi ya silaha za Magharibi katika maeneo ya Bryansk na Kursk.
Putin ameusifu mfumo mpya wa silaha wa Urusi kama wa kipekee, akisema wakati unapotumiwa pamoja, nguvu yake ya uharibifu inaweza kulinganishwa na ile ya bomu la nyuklia.
Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, amesema matumizi ya kombora hilo na Urusi ni juhudi za kuvuruga jitihada za amani zinazotarajiwa kufanywa na Rais Mteule wa Marekani, Donald Trump.