1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
UchumiChina

Putin akutana na Xi Jinping katika mkutano wa mradi wa BRI

17 Oktoba 2023

Rais Xi Jingping wa China amemkaribisha rais wa Urusi Vladmir Putin mjini Beijing mwanzoni mwa mkutano wa kilele wa mradi wa Belt and Road Initiative (BRI)

Rais wa Urusi Vladimir Putin (Kushoto) na mwenzake wa China Xi Jinping (Kulia) wazungumza pembezoni mwa mkutano wa BRI mjini Beijing mnamo Oktoba 17, 2023
Rais wa Urusi Vladimir Putin (Kushoto) na mwenzake wa China Xi Jinping (Kulia)Picha: Sergey Savostyanov/Sputnik/AP/picture alliance

Anayeongoza orodha ya wageni wanaohudhuria mkutano huo wa mradi wa kimataifa wa China wa ujenzi wa miundo mbinu ya usafiri wa reli na barabara, Belt and Road Initiative (BRI) ni rais Putin ambaye yuko katika ziara yake ya kwanza kwa taifa lenye nguvu duniani tangu uvamizi wa Urusi nchini Ukraine kusababishwa kutengwa kwa serikali yake kimataifa. Viongozi hao wawili wamekutana Jumanne (17.10.2023) katika hafla ya ufunguzi wa mkutano huo huku video iliyochapishwa na wizara ya mambo ya nje ya Urusi ikiwaonesha wakisalimiana. Wawili hao pia walipiga picha ya pamoja na viongozi wengine wanaohudhuria mkutano huo.

Putin kufanya mazungumzo na Xi Jinping siku ya Jumatano

Ikulu ya Kremlin imesema kuwa Putin anatarajiwa kufanya mazungumzo ya kina na Xi pembezoni mwa mkutano huo Jumatano (17.10.2023), huku vita vinavyoendelea kati ya Israel na kundi la Hamas likiwa suala la kipaombele katika mkutano huo. Ikulu ya Kremlin imeendelea kusema kuwa wakati wa mazungumzo hayo kipaumbele maalum kitatolewa kwenye masuala ya kimataifa na kikanda bila ya kutoa maelezo zaidi.

Putin analenga kuimarisha uhusiano zaidi na China

Mjini Beijing, Putin yuko katika harakati ya kuimarisha uhusiano ambao tayari ni mzuri kati ya mataifa hayo mawili, ingawa wataalamu wanasema Urusi inazidi kuwa mshirika mdogo katika uhusiano huo.

Soma pia: Kenya yasaka mikopo zaidi kutoka China

Wakati huo huo,  China imesema itafuata kanuni ya ustahimilivu wa madeni katika kufadhili miradi ya BRI.

Treni ya kubebea mizigo ya mradi wa reli ya kisasa ya SGR kutoka Mombasa kuelekea Nairobi nchini KenyaPicha: Wang Teng/Xinhua/picture alliance

Makamu wa waziri mkuu wa China He Lifeng amesema kuwa China iko tayari kushirikiana na pande zote kuzingatia uwazi na uhusiano, kujenga miundombinu bora zaidi ya usafiri wa baharini, anga na barabara. Ameongeza kwamba wanataka watu kufurahia usafirishaji mzuri wa bidhaa, na kuweka hali bora na rahisi zaidi ya ubadilishanaji wa bidhaa na watu.

China yatafuta kuimarisha ushirikiano na utawala wa Taliban

Katika hatua nyingine, China imetafuta kuimarisha ushirikiano wake rasmi na utawala wa Taliban tangu kuondoka kwa wanajeshi wa  Marekani na vikosi vingine vya kigeni nchini humo miaka miwili iliyopita licha ya utawala huo kukosa kutambuliwa rasmi na nchi yoyote.

Msemaji wa ubalozi wa China ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba Kaimu waziri huyo wa biashara wa utawala Azizi aliwasili mjini Beijing katika saa za mchana.

Afghanistan inatarajia kuhakikisha utulivu na maendeleo ya kiuchumi

Wizara ya mambo ya nje ya China imesema kuwa nchi hiyo imebainisha kuwa serikali ya mpito ya Afghanistan imesema inatarajia kuchukua fursa hiyo ya mradi wa BRI na kuhakikisha utulivu wa kitaifa na maendeleo ya kiuchumi haraka iwezekanavyo.

Msemaji wa wizara ya biashara ya China amesema kuwa Azizi atavutia wawekezaji wakubwa na kuendeleza mazungumzo na maafisa wa China kuhusu mipango ya kujenga barabara kupitia ukanda wa  Wakhan kaskazini mwa nchi hiyo.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW