1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Putin amteuwa kamanda wa Wagner kuandaa wapiganaji Ukraine

29 Septemba 2023

Rais Vladimir Putin wa Urusi amemteuwa mmoja kati ya makamanda wa juu wa makandarasi wa kijeshi wa Wagner kuongoza kile Kremlin inachokiita "vikosi vya kujitolea" kupigana vita nchini Ukraine.

Russland Moskau | Yunus-Bek Yevkurov und Col. Andrey Troshev (Ausschnitt Troshev)
Picha: Mikhail Metzel/ITAR-TASS/IMAGO

Kupitia tamko lililotolewa na ikulu ya Kremlin siku ya Ijumaa (Septemba 29), Putin alimuambia Andrei Troshev kwamba jukumu lake la sasa ni kushughulikia "kuundwa kwa vikosi vya wapiganaji wa kujitolea" vinavyoweza kutekeleza majukumu mbalimbali ya kivita, hasa kwenye eneo lililo katika "operesheni maalum ya kijeshi", akimaanisha vita vyake nchini Ukraine. 

Naibu Waziri wa Ulinzi, Yunus-Bek Yevkurov, alihudhuria pia mkutano uliofanyika jioni ya Alkhamis (Septemba 28), ishara kuwa mamluki wa Wagner wataendelea kuhudumu chini ya wizara yake.

Soma zaidi: Je, Rais Putin wa Urusi bado ana nguvu kiasi gani?

Akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari siku ya Ijumaa, msemaji wa Kremlim, Dmitry Peskov, alithibitisha kwamba Troshev sasa anaifanyia kazi wizara ya ulinzi na akataka masuali juu ya uwezekano wa wapiganaji wa Wagner kurejea Ukraine yaelekezwe kwa wasemaji wa jeshi.

Nafasi nyengine ya Wagner

Wapiganaji wa Wagner hawakuwa na jukumu lolote muhimu kwenye mstari wa mbele wa mapambano tangu walipojiondowa baada ya kuuteka mji wa mashariki mwa Ukraine wa Bakhmut kufuatia vita vya muda mrefu na vilivyopoteza idadi kubwa ya wapiganaji wa pande zote.

Kamanda wa kundi la Wagner, Andrei Troshev (kulia) akiwa na Naibu Waziri wa Ulinzi wa Urusi, Yunus-Bek Yevkurov.Picha: Mikhail Metzel/Pool/SPutnik/REUTERS

Lakini mkutano huo kati ya uongozi wa kundi hilo na Rais Putin katika Ikulu ya Kremlin unaashiria mipango ya serikali ya Urusi kuwarejesha wapiganaji hao mstari wa mbele wa mapambano nchini Ukraine, baada ya uasi wao uliodumu kwa muda mfupi mwezi Juni na kifo chenye utata cha Prigozhin tarehe 23 Agosti.

Soma zaidi: Urusi yasema haitochunguza ajali ya ndege iliyomuua Prigozhin

Wachambuzi wanasema kikosi hicho chenye maelfu ya wapiganaji ni jeshi lenye thamani kubwa ambalo Kremlin haiwezi kuliwacha bila kulitumia.

Uingereza yaongeza vikwazo

Hayo yakijiri, serikali ya Uingereza imetangaza hivi leo vikwazo vipya dhidi ya maafisa wa Urusi waliohusika na uchaguzi ulioiwezesha Urusi kuyanyakuwa majimbo matano ya Ukraine: Zaporizhzhia, Kherson, Luhansk, Donetsk na Crimea. 

Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak (kushoto) akiwa na Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine.Picha: Paul Ellis/AP/picture alliance

London inasema maafisa hao waliowekewa vikwazo walishiriki kwenye kile ilichokiita "chaguzi za aibu" kwenye majimbo hayo. 

Soma zaidi: Uingereza inapanga kulipiga marufuku kundi la Wagner

"Uingereza kamwe haitatambuwa kwamba Urusi ndiyo yenye mamlaka kwenye majimbo iliyoyanyakuwa kutoka Ukraine. Crimea, Zaporizhzhia, Donetsk, Luhansk na Kherson ni Ukraine." Ilisema taarifa ya Wizara ya Mambo ya Kigeni wa Uingereza.

Vile vile, vikwazo hivyo vya Uingereza ambavyo vinajumuisha kushikilia mali za maafisa hao, vinawahusu pia Waziri wa Masuala ya Dharura wa Urusi, Alexander Kurenkov, na Kamishna Mkuu wa Uchaguzi wa Urusi, Natalya Budarina.

Vyanzo: AP, Reuters
 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW