Putin: Kilichofanywa na Wagner ni uhaini
24 Juni 2023Ameyasema hayo baada ya kiongozi wa kampuni ya mamluki wa kijeshi ya Wagner Yevgeny Prighozin kutangaza kuwa wapiganaji wake, sasa wanadhibiti makao makuu muhimu ya kijeshi yanayoshughulikia mashambulizi dhidi ya Ukraine.
Matukio haya yanayoendelea kwa kasi yanatoa changamoto kubwa kwa utawala wa Rais Putin na hatari kubwa ya kiusalama tangu alipoingia madarakani mwaka 1999. Mkuu wa kundi la Wagner, Prighozin, awali alisema kuwa wapiganaji wake wanadhibiti kituo cha amri za kijeshi na kambi ya anga kwenye mji wa kusini wa Rostov-on-Don na aliapa kuwapindua viongozi wajuu wa jeshi la Urusi.
Makao hayo makuu muhimu kijeshi ya Urusi ya mjini Rostov-on-Don ni ngome muhimu ya mashambulizi dhidi ya Ukraine. Baaadhi ya Picha na video zilizochapishwa mtandaoni na vyombo mbalimbali vya habari likiwemo shirika la habari la TASS la Urusi liliwaonesha watu waliobeba silaha wakiwa wameyazunguka majengo ya Utawala mjini Rostov na magari ya kivita yakipelekwa katikati ya mji. Hata hivyo haikuwa wazi kuwa watu hao waliobeba silaha ni wa upande upi.
Akihutubia kwa njia ya televisheni Rais Putin alimjibu kiongozi huyo wa Wagner aliyekuwa mshirika wake - ambaye jeshi lake binafsi alisaidia kuipa Urusi baadhi ya vikosi muhimu katika mashambulizi dhidi ya Ukraine na kusema alichokifanya ni usaliti unaotishia uhai wa taifa la Urusi.
Ameongeza kuwa katika mapambano yanayoendelea dhidi ya Ukraine, Urusi inahitaji umoja wa vikosi vyote. Putin amesema wanakabiliwa na usaliti wa hali ya juu, matamanio kupita kiasi na maslahi binafsi ambayo yanaweza kusababisha uhaini.
Rais huyo wa Urusi ameongeza kuwa wote waliohusika na usaliti na kuandaa uasi wa kijeshi wataadhibiwa. Tayari Meya wa mjini Moscow ameshatangaza kuwa hatua zote za kupambana na ugaidi zinaendelewa kuchukuliwa katika mji huo muu na kwamba usalama umeimarishwa kwenye maeneo kadhaa.
Prighozin asema kamwe hatojisalimisha kwa Putin
Baada ya hotuba ya leo Jumamosi ya Rais Putin, mkuu wa kundi la mamluki wa Wagner amenukuliwa akisema kuwa yeye na wapiganaji wake hawatojisalimisha kwa amri ya Putin. Prigozhin amesema Rais Putin anafanya kosa kubwa kumtuhumu yeye na kundi lake kwa usaliti.
Amesisitiza wao ni wazalendo wa nchi yao, wamepgana na wataendelea kupigana kwa ajili ya Urusi. Ameongeza kuwa hawataki nchi hiyo iendelee kwenye rushwa, udanganyifu na urasimu.
Soma zaidi:Kremlin yakanusha ripoti kuwa Mkuu wa Wagner alikuwa tayari kuisaliti Urusi
Akitoa kauli yake kwa njia ya mitandao ya kijamii juu ya yanayoendelea Urusi Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky mapema leo amesema uasi wa kijeshi wa kundi la mamluki la Wagner ni ushahidi wa Urusi kutokuwa na utulivu wa kisiasa. Amesema, udhaifu wa Urusi ni dhahiri na kwamba kadri nchi hiyo itakavyoendelea kuwaacha wanajeshi wake Ukraine, ndivyo itakavyozidi kukabiliwa na mparaganyiko, maumivu na matatizo yatakayoikumba baadaye.
Itakumbukwa kuwa, kundi la mamluki la Wagner linalotuhumiwa kwa uasi wa kijeshi Urusi, limekuwa likihusishwa kufanya operesheni zake katika baadhi ya mataifa ya Afrika yakiwemo Mali na Sudan.