1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Putin aonya dhidi ya majaribio ya kuishinda Urusi

24 Oktoba 2024

Rais wa Urusi, Vladimir Putin, aliandaa mkutano wa kilele wa BRICS akiwakaribisha Rais wa China Xi Jinping, Waziri Mkuu wa India Narendra Modi, na viongozi wengine.

Urusi, Moscow | Vladimir Putin mkutano wa BRICS
Putin aliikosoa Marekani kwa kutumia vibaya dola kama silaha na alipendekeza kuundwa kwa jukwaa la uwekezaji la BRICSPicha: Alexander Zemlianichenko/AFP

Ulihusu ushirikiano wa kifedha, mifumo mbadala ya malipo kwa ile inayotawaliwa na Magharibi, utatuzi wa migogoro ya kikanda na kutanua kundi la BRICS. Putin atakutana na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres,kwa mara ya kwanza baada ya zaidi ya miaka miwili, ambapo wanatarajiwa kujadili mgogoro wa Ukraine na mzozo wa Mashariki ya Kati huku kukiwa na shinikizo kutoka kwa washirika wa BRICS kumaliza vita. 

Soma pia: BRICS yataka vita vikomeshwe Gaza, Ukraine

Mkutano huo wa siku tatu unaofanyika katika jiji la Kazan unahudhuriwa na nchi 36Picha: WENDYS OLIVO/AFP

Mkutano huo wa siku tatu unaofanyika katika jiji la Kazan ulioanza Jumanne unahudhuriwa na nchi 36, ukionyesha kushindwa kwa juhudi zinazoongozwa na Marekani kuitenga Urusi kutokana na uvamizi wake nchini Ukraine. Kremlin imeutaja mkutano huo kama "tukio kubwa zaidi la sera ya kigeni kuwahi kufanywa" na inauona BRICS kama mbadala kwa mfumo wa utawala wa dunia unaohodhiwa na mataifa ya Magharibi, huku ikiimarisha juhudi za kuvutia nchi zenye kipato kidogo na cha kati baada ya kutuma wanajeshi Ukraine mwezi Februari 2022.

Soma pia: Modi amuambia Putin akaye kitako na Zelensky

Putin aliikosoa Marekani kwa kutumia vibaya dola kama silaha na alipendekeza kuundwa kwa jukwaa la uwekezaji la BRICS ili kusaidia uchumi na kutoa rasilimali kwa nchi za Kusini na Mashariki ya Dunia. Pia, alisisitiza kuwa nchi za BRICS zinashiriki maadili ya amani, haki, na usawa, na zinajitahidi kuchangia katika kuunda mpangilio wa haki wa dunia wenye ushiriki wa nchi za Kusini na Mashariki katika utawala wa kimataifa. Majadiliano yalionyesha tena kuwa nchi za BRICS zinashiriki maadili ya ulimwengu ya amani, haki, na usawa, na zinashirikiana kwa ustawi wa nchi na watu wao. Nchi za BRICS zimesimama pamoja kuunga mkono kuimarisha ushirikiano duniani kwa misingi ya kanuni kuu za Mkataba wa UN, na zinajitahidi kuchangia kwa kila njia katika kuunda mpangilio wa haki wa dunia wenye ushiriki muhimu wa nchi za Kusini na Mashariki ya Dunia.

Wakuu wa mataifa wakutana Kazan kwenye BRICS

01:42

This browser does not support the video element.

Katika tamko la pamoja, washiriki wa mkutano huo walieleza wasiwasi wao kuhusu "athari mbaya za hatua za kulazimisha zisizo halali, ikiwemo vikwazo haramu" na wakasisitiza dhamira yao ya kuimarisha ushirikiano wa kifedha ndani ya BRICS, huku wakizingatia manufaa ya zana za malipo ya mpakani ambazo ni za haraka, gharama nafuu, salama, na jumuishi.

Jumatano, Xi alisisitiza jukumu la BRICS katika kuhakikisha usalama wa dunia, akieleza kuwa lazima wafanye kazi pamoja kuimarisha mshikamano wa mataifa ya Kusini na kuwa mstari wa mbele katika mageuzi ya utawala wa kimataifa, huku akibainisha kwamba China na Brazil zimependekeza mpango wa amani kwa Ukraine, ingawa Ukraine imeukataa.

Putin anatarajiwa kukutana na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, ambaye amekuwa akikosoa vikali hatua za Moscow nchini Ukraine, huku ziara yake nchini Urusi kwa mara ya kwanza baada ya zaidi ya miaka miwili ikizua hasira kutoka Kyiv.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Ukraine ilisema kuwa ziara hiyo ni "chaguo lisilofaa" linaloharibu sifa ya Umoja wa Mataifa, lakini msemaji wa Guterres, Farhan Haq, alijibu kwa kusema kuwa mkutano huo ni sehemu ya utaratibu wa kawaida kuhudhuria mikutano muhimu ya mashirika yenye wanachama wengi muhimu kama BRICS.