Putin asema malengo ya uvamizi dhidi ya Ukraine yatatimizwa
27 Aprili 2022Hayo Putin ameyasema leo katika hotuba aliyoitoa mbele ya bunge mjini Moscow. Amesema kufanikishwa kwa uvamizi dhidi ya Ukraine, anaoutaja kama operesheni ya kijeshi, kutahakikisha usalama kwa wakaazi wa majimbo mawili yaliyojitenga mashariki mwa Ukraine, ambayo Putin aliyatambua kama nchi huru kabla ya kuamuru uvamizi huo wa tarehe 24 Februari.
Soma zaidi: Biden amtuhumu Putin kwa mauaji ya halaiki nchini Ukraine
Kuhusiana na mzozo huo wa vita, kwa mara ya kwanza Ukraine imedokeza juu ya uwezekano wa kuhusika kwake katika miripuko ambayo imekuwa ikitokea katika mikoa ya Urusi iliyo karibu na Ukraine mnamo siku za hivi karibuni.
Ukraine kuhusika na miripuko nchini Urusi
Hii leo gavana wa mkoa wa Urusi wa Belgorod amethibitisha kuwa bohari moja la silaha limeshika moto baada ya kiripuko kdhaa kusikika, na katika kile kinachochukuliwa kama jibu kwa taarifa hiyo, Mykhailo Podolyak ambaye ni mshauri wa rais wa Ukraine, ameandika katika mtandao wa Telegram, akisema na hapa namnukuu, ''Karma ni kitu kinachoumiza'', hapo akimaanisha kuwa matendo mabaya hulipwa kwa mabaya.
Soma zaidi: Miji ya kusini mwa Ukraine yashambuliwa na Urusi
Afisa huyo wa Ukraine ameongeza katika ujumbe wake, kuwa wakaazi wa maeneo ya Urusi yaliyoathirika, wanaanza kuonja ladha ya dhana ya ''kuondoa shughuli za kijeshi'', akikejeli sababu iliyotajwa na Putin wakati alipoamuru uvamizi dhidi ya Ukraine.
Wakati huo huo, mikutano na mashauriano vimekuwa vikiendelea katika nchi za Umoja wa Ulaya, baada ya Urusi kuzifungia Poland na Bulgaria mgao wa gesi, kufuatia hatua ya nchi hizo kukataa kulipia huduma hiyo kwa sarafu ya Urusi ya Ruble kama ilivyoamuliwa na rais Vladimir Putin.
Urusi kuifunga gesi yake ni uchokozi-Von der Leyen
Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen amesema hatua hiyo ya Urusi ni ya uchokozi, na kuongeza kuwa hivi sasa Poland na Bulgaria zinapata mgao wa gesi kutoka wanachama wengine wa Umoja wa Ulaya.
Hali kadhalika, katika kuonyesha mshikamano na nchi hizo mbili, Bi von der Leyen amezionya nchi nyingine za Umoja wa Ulaya zilizo tayari kulipia gesi ya Urusi kwa sarafu ya Ruble, kuwa zitakuwa zikikiuka vikwazo vya umoja huo.
Soma zaidi: Ulaya haitonunua gesi ya Urusi kwa sarafu ya taifa hilo
Ujerumani ambayo inapata zaidi ya asilimia 40 ya mahitaji yake ya gesi kutoka Urusi, waziri wake wa uchumi Robert Habeck amesema katika mazingira yaliyopo, haondoi uwezekano wa kuvitaifisha viwanda vya Urusi vilivyoko Ujerumani, akiongeza kuwa serikali mjini Berlin inajiandaa kwa mipango ya kisiasa ambayo haijawahi kutafakari siku za nyuma.
ape,rtre