1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Putin asema Marekani na NATO zimepuuza matakwa ya Urusi

Admin.WagnerD28 Januari 2022

Vladimir Putin amemwambia mwenzake wa Ufaransa Emmanuel Macron kwamba Marekani na washirika wake katika NATO hawakuzingatia matakwa ya kiusalama ya Urusi kwenye majibu waliyowasilisha wiki hii. 

Russlands Präsident Wladimir Putin
Picha: Mikhail Metzel/SPUTNIK/AFP

Ni mgogoro ambao umeendelea kutokota huku wasiwasi ukisababishwa na mrundiko wa zaidi ya wanajeshi 100,000 wa Urusi karibu na mpaka wake na Ukraine. Nchi za magharibi zikihofia Urusi inapanga uchokozi wa kuivamia Ukraine.

Kulingana na taarifa iliyotolewa na ikulu ya rais wa Urusi, rais Vladimir Putin amemwambia mwenzake wa Ufaransa Emmanuel Macron kwamba Marekani na washirika wake wa magharibi hawakutilia maanani matakwa ya msingi ya Urusi ikiwemo kutaka NATO iache kujitanua, na kuacha kupeleka zana za mashambulizi karibu na mpaka wa Urusi.

Urusi: Majibu ya Marekani kuhusu Ukraine hayaridhishi

Putin amemuelezea Macron kwamba Marekani ilishindwa kueleza ni vipi wanaweza kuhakikisha usalama wa Ulaya pasi ya kuathiri au kuhujumu  matakwa ya kiusalama ya nchi nyingine.

Kulingana na serikali ya Ufaransa, dhamira ya Emmanuel Macron katika mazungumzo na Vladimir Putin ni kujua msimamo wa Urusi kuwapeleka wanajeshi wake mpakani na Ukraine na pia kuhimiza mazungumzo.Picha: Ludovic Marin/REUTERS

Ikulu ya Putin imesema marais hao walizungumza kwa muda mrefu, huku Putin akimwambia Macron kwamba atayatathmini kwa undani majibu ya Marekani na NATO, kisha baadaye atafanya maamuzi kuhusu hatua atakazochukua.

Macron na Putin kutafuta suluhisho la mzozo wa Ukraine

Hapo awali, waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov alisema Urusi haitaki vita, lakini haitakubali matakwa yake kupuuzwa.

Katika mahojiano na idhaa za redio nchini Urusi, Lavrov amesisitiza kuwa hawataruhusu matakwa yao kupuuzwa.

Miongoni mwa matakwa ya Urusi yalikuwa ni pamoja na marufuku kwa Ukraine kujiunga na NATO na pia wawe na kambi mpya za kijeshi katika nchi za zamani za kisoviet.

Marekani na NATO zimepinga matakwa hayo huku Marekani ikiainisha masuala ambayo pande husika zinaweza kushiriki mazungumzo ili kuepusha vita.

Mrundiko wa vikosi vya kijeshi vya Urusi karibu na mpaka na Ukraine, wazusha wasiwasi kwamba Urusi yapamba kuivamia Ukraine.Picha: AP/picture alliance

Lavrov aliongeza kwamba kuweka vikwazo binafsi dhidi ya Putin na Urusi mfano vikwazo katika mfumo wa malipo ya kifedha, kutakuwa kama kuvunja uhusiano na Urusi. Na hafikirii kama kuna yeyote anayetaka kuchukua hatua hiyo.

Sintofahamu yaendelea kugubika mazungumzo kuhusu Ukraine

Mnamo Alhamisi, rais wa Marekani Joe Biden alimtahadharisha rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy kuhusu uwezekano mkubwa wa Urusi kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya nchi yake mwezi Februari.

Wakati Urusi na nchi za magharibi zikitafakari hatua ya kuchukua, NATO imesema inaimarisha ulinzi wake katika ukanda wa bahari ya Baltic.

Kwa upande wake Urusi imeanzisha misururu ya luteka kadhaa za kijeshi zikihusisha matumizi ya zana nzito za vita kusini magharibi mwa Urusi, ndege za kivita, manowari na zana nyingine za vita.

(AP, AFP)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW