1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUrusi

Urusi yasaini makubaliano ya kijeshi na mataifa ya Afrika

29 Julai 2023

Rais wa Urusi Vladmir Putin ametangaza kuwa nchi yake imetia saini makubaliano ya ushirikiano wa kijeshi na zaidi ya nchi 40 za Afrika.

2nd Russia-Africa Summit: plenary session
Picha: Mikhail Tereshchenko/TASS/dpa/picture alliance

Putin amesema haya jana siku ya pili na ya mwisho ya mkutano wa pili wa kilele wa Urusi na viongozi wa Afrika. Putin amesema kwa madhumuni ya kuimarisha uwezo wa mataifa ya Afrika, wanapanga ushirikiano wa kijeshi na nyanja za kiufundi za kijeshi. Putin amesema mataifa ya Afrika yalipokea silaha mbalimbali na teknolojia, baadhi bila malipo, kwa lengo la kuimarisha usalama na uhuru wa mataifa hayo. Wawakilishi kutoka nchi za Afrika wamealikwa kushiriki kikamilifu katika mikutano ya kijeshi ilioandaliwa na Urusi inayoshughulikia masuala ya kiufundi ya silaha hizo na kupata mafunzo kuvielewa vifaa hivyo na matumizi yake.

Urusi itaendelea kuwa msambazaji wa kutegemewa wa nafaka

Putin alisisitiza kuwa Urusi itaendelea kuwa msambazaji wa kutegemewa wa nafaka kwa nchi za bara Afrika. Ahadi hiyo ilikuja baada ya Urusi kujiondoa katika mkataba ambao uliruhusu nafaka za Ukraine kuuzwa nje kupitia Bahari Nyeusi. Ukraine ni muuzaji mkuu wa nafaka barani Afrika.

Umoja wa Afrika wataka kufikia usitishaji wa mapigano

Katika hotuba yake ya kufunga mkutano huo wa kilele, mwenyekiti wa Umoja wa Afrika Azali Assoumani, amesema pendekezo la Putin la kutoa nafaka halitoshi. Assoumani amesema hatua hiyo ni muhimu lakini huenda isitoshe kufanya hivyo akiongeza kwamba kile wanahitaji kuafikia ni usitishaji wa mapigano. Kiongozi huyo ya Umoja wa Afrika amesema kuwa rais Putin ameonesha kuwa yuko tayari kushiriki katika mazungumzo na kutafuta suluhisho na kwamba sasa wanahitaji kuushawishi upande wa pili.

Rais wa Urusi Vladmir Putin akiwa na rais wa Umoja wa Afrka Azali Assoumani (Katikati) na mwenyekiti wa kamisheni ya Umoja wa Afrika Moussa Faki MahamatPicha: Mikhail Tereshchenko/AFP

Urusi pia inalenga kupanua uwepo wake barani Afrika kwa kufungua balozi mpya na kuongeza wafanyakazi wake katika uwakilishi wa diplomasia zilizopo.

Putin asema yuko tayari kufanya mazungumzo kuhusu Ukraine

Baada ya miito ya amani nchini Ukraine wakati wa kongamano hilo, Putin alisisitiza nia yake ya kufanya mazungumzo kuhusu Ukraine. Hata hivyo Putin amesema kuwa hakuna njia ya kulazimisha upande wowote katika mazungumzo kama hayo. Mshauri wa rais wa Ukraine Mykhailo Podolyak, amekosoa matamshi hayo ya Putin na kusema haina maana kwasasa kwa  Ukraine kufanya mazungumzo na Urusi.

Putin atafuta kuonesha hajatengwa kimataifa

Wakati wa mikutano na wakuu wa nchi na serikali wa Afrika wakati wa kongamano hilo, Putin alitaka kuonyesha kwamba hajatengwa kimataifa. Kulingana na ikulu ya Kremlin, nchi 49 kati ya 54 za bara Afrika zimewakilishwa, huku 17 tu wakiwa wakuu wa nchi au serikali, hii ikiwa idadi ya chini ikilinganishwa na kongamano la kwanza la mwaka 2019.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW