vita dhidi ya magaidi
18 Desemba 2015Rais Putin alisisitiza kwenye mkutano na waandishi wa habari , unaofanyika kila mwaka, kwamba Urusi inashirikiana na Marekani nchini Syria.
Hata hivyo kwa mara nyingine aliinawa Uturuki na kusema kuwa serikali ya nchi hiyo inajikomba kwa Marekani . Amesema haoni iwapo pana uwezekano wa kuufanya uhusiano baina ya Urusi na serikali ya Uturuki uwe mzuri.
Putin amefahamisha kuwa Urusi inawasiliana na baadhi ya wapinzani wa Syria lakini bila ya kuwataja wapinzani hao.
Kiongozi huyo wa Urusi anaeitwa mwamba, na vyombo vya habari vya magharibi, aliitumia fursa ya mkutano na waandishi wa habari mjini Moscow kusisitiza kwa mara nyingine kwamba mashambulio ya ndege za Urusi yanawalenga magaidi wa dola la kiislamu, kinyume na madai yanayotolewa na nchi za magharibi kwamba Urusi inawashambulia wapinzani wa Assad.
Putin ameeleza kuwa inawezekana kuleta suluhisho la kisiasa nchini Syria. Lakini amesisitza kuwa ni watu wa Syria tu wenye haki ya kuchagua wa kuwaongoza.
Rais Vladimir Putin ameyatamka hayo siku moja kabla ya kufanyika, mjini New York kwa mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa nchi 17, ikiwa pamoja na kutoka Urusi,Iran na Saudi Arabia zinazohesbaika kuwa na uzito wa juu katika mgogoro wa nchini Syria.
Mawaziri hao watakutana kwa ajili ya duru ya tatu ya mazungumzo juu ya kuumaliza mgogoro wa Syria. Kwenye mkutano wao wa hivi karibuni, mawaziri hao walikubaliana juu ya kufanyika mazungumzo ya amani , yatakayoongozwa na Umoja wa Mataifa na ikiwezekana kusimamisha mapigano mnamo mwezi wa Januari.
Wakati huo huo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linatazamiwa kuwasilisha mswada wa azimio juu ya kuzifunga njia za kuingizia fedha zinazotumiwa magaidi wa dola la kiislamu .Putin ameahidi kuwa Urusi itauunga mkono mswada huo.
Kwenye mkutano wake na waandishi wa habari mjini Moscow Rais Putin pia alizungumzia juu ya masuala ya FIFA, na kampeni za kuwania nafasi ya kugombea urais nchini Marekani.
Mwandishi:Mtullya Abdu./afp,
Mhariri:Iddi Ssessanga