1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Putin ashinda muhula wa nne madarakani

Caro Robi
19 Machi 2018

Rais wa Urusi Vladimir Putin ameshinda kwa urahisi katika uchaguzi uliofanyika Jumapili kwa kupata asilimia 76.6 ya kura na hivyo kumhakikishia muhula wa nne madarakani licha ya upinzani kudai kulikuwa na udanganyifu.

Moskau Präsidentschaftswahlen Ansprache Putin
Picha: AP/D. Tyrin

Akiwahutubia wafuasi wake mjini Moscow, baada ya ushindi huo, Putin amesema matokeo hayo ni ishara ya kutambua kile ambacho wameweza kutimiza katika kipindi cha miaka michache iliyopita licha ya mazingira magumu.

Akiongeza kuwa sasa wanaelekeza mawazo yao kuelekea siku za usoni za taifa lao na mustakabali wa siku za baadaye wa watoto wao.

Upinzani wadai uchaguzi ulikumbwa na udanganyifu

Kulingana na tume ya kitaifa ya uchaguzi, mpinzani wake wa karibu Pavel Grudinin wa chama cha Kikomunisti amepata asilimia 12 ya kura. Vladimir Zhirinovsy alipata asilimia sita, Ksenia Sobchak alipata asilimia 1.5 na wagombea wengine wanne walipata chini ya asilimia moja ya kura zilizopigwa.

Kiongozi wa Upinzani nchini Urusi Alexei NavalnyPicha: picture-alliance/abaca/A. Finistre

Kulikuwa na wagombea saba waliowania urais dhidi ya Putin lakini mpinzani wake mkuu Alexei Navalny alizuiwa na tume ya uchaguzi kugombea. Ushindi huo wa zaidi ya asilimia 76 ulitarajiwa na wengi kwani Putin hakuwa na mshindani mwenye ushawishi. Grudinin amesema uchaguzi ulikumbwa na udanganyifu.

Navalny ambaye aliwataka wafuasi wake kuususia uchaguzi huo alioutaja bandia alituma waangalizi 3,000 kote nchini kufuatilia idadi ya wapiga kura waliojitokeza kushiriki uchaguzi na kulinganisha na matokeo ya waangalizi wengine amesema kulikuwa na dosari kubwa katika uchaguzi.

Upinzani umedai kulikuwa na udanganyifu katika uchaguzi huo huku kundi la waangalizi wa uchaguzi la Urusi likipokea malalamiko kadhaa na kuripoti kulikuwa na zaidi ya visa 2,500 vya udanganyifu wa kura kote nchini. Tume ya uchaguzi imepuuzilia mbali madai hayo kwa kusema saa nyingine waangalizi hutathmini mambo visivyo. Kiasi ya Warusi milioni 107 walisajiliwa kama wapiga kura.

Putin asema hatakuwa Rais wa milele

Rais wa China Xi Jinping amempongeza Putin ambaye ameiongoza Urusi kwa takriban zaidi ya miongo miwili kwa ushindi huo akisema China iko tayari kushirikiana na Urusi kuimarisha zaidi uhusiano mzuri uliopo kati ya nchi hizo mbili.

Rais wa Urusi Vladimir PutinPicha: Getty Images/AFP/S. Chirikov

Uchaguzi huo umefanyika wakati Urusi ikizidi kutengwa na nchi za magharibi kufuatia kadhia ya hivi karibuni ya kupewa sumu kwa jasusi wa zamani wa Urusi Sergei Skripal nchini Uingereza na duru mpya ya vikwazo kutoka kwa Marekani huku taifa hilo likijiandaa kuwa mwenyeji wa mashindano ya soka ya kuwania kombe la dunia mwaka huu.

Tangu kuchaguliwa kwa mara ya kwanza kuwa rais mwaka 2000, Putin amedhihirisha nguvu zake katika kuliongoza taifa hilo kubwa zaidi duniani, kukandamiza upinzani, vyombo vya habari na kuifanya Urusi kuzidi kuwa dola lenye nguvu katika safu ya kimataifa kwa kuusaidia kijeshi utawala wa Syria na kulichukua eneo la Crimea nchini Ukraine. Putin ambaye amesisitiza hanuui kusalia madarakani milele, amesema atatumia muhula wake wa nne kushughulia matatizo chungu nzima yanayoikumba nchi yake ikiwemo umasikini, ukosefu wa ajira na kuimarisha huduma za afya.

Mwandishi: Caro Robi/afp/ap

Mhariri: Iddi Ssessanga

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW