1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Putin atishia kusitisha usambazaji wa gesi kwenda Ulaya

7 Septemba 2022

Rais wa Urusi Vladimir Putin amesema anataka kujadili juu ya mkataba uliosimamiwa na Umoja wa Mataifa wa kuiruhusu Ukraine kusafirisha nafaka zake katika soko la kimataifa kupitia bandari ya bahari nyeusi.

Russland | Wladimir Putin beim Eastern Economic Forum (EEF) in Wladiwostok
Picha: Sergey Bobylev/TASS Host Photo Agency/REUTERS

Putin ametishia pia kusitisha kabisa usambazaji wa nishati kwenda Ulaya iwapo Umoja wa Ulaya utaweka ukomo na hatimaye kushusha bei ya gesi ya Urusi. 

Katika hotuba iliyokuwa na hisia kali aliyoitoa kwenye kongamano la kiuchumi katika eneo la Mashariki mwa Urusi, Putin hakuzungumzia sana kuhusu uvamizi wa jeshi la nchi hiyo nchini Ukraine, japo amesisitiza kuwa kamwe Urusi haitoshindwa vita hivyo. Rais huyo ameeleza kuwa Urusi imeimarisha utawala na kupanua ushawishi wake.

Soma pia:Urusi yanyemelewa na vikwazo vingine vikali kutoka Magharibi

Mkataba huo wa usafirishaji wa nafaka, uliosimamiwa na Umoja wa Mataifa na Uturuki, uliwezesha kufunguliwa kwa njia salama za kusafirisha nafaka kupitia bahari nyeusi kwa bidhaa za Ukraine baada ya serikali ya mjini Kiev kupoteza njia zake za usafirishaji wa bidhaa kupitia ardhi, anga na bahari baada ya uvamizi wa Urusi.

Mkataba huo ambao uliwekwa mahsusi kwa ajili ya kusaidia kupunguza bei za vyakula duniani, ndio mafanikio ya kipekee ya kidiplomasia kati ya Urusi na Ukraine kwa zaidi ya miezi sita ya vita.

Bwana Putin hata hivyo, amesema kinyume na makubaliano yao ya awali, mpango huo wa usafirishaji wa nafaka umekuwa ukisafirisha vyakula na mbolea kwa mataifa mengine ya Umoja wa Ulaya pamoja ya Uturuki badala ya nchi maskini ambazo ndizo zilizokuwa zimepewa kipau mbele.

Kutokana na hali hiyo, Rais huyo wa Urusi sasa amesema anataka kubadilisha masharti ya mkataba huo.

Kauli yake imeibua uwezekano wa makubaliano kuingia doa iwapo pande zote zitashindwa kuafikiana juu ya masharti mapya au hata unaweza kufutwa baada ya muda wake kukamilika mwishoni mwa mwezi Novemba.

Soma pia: Von der Leyen: Mianya mikubwa ingalipo kuhusu Brexit

Lakini kwa upande wa Ukraine, ambayo bandari zake zimezuiwa na Urusi, imesema masharti ya mkataba huo uliotiwa saini mnamo Julai 22 kwa muda wa miezi minne, yalikuwa yakizingitwa kwa uangalifu mkubwa na kwamba hakukuwa na sababu za kuujadili upya.

EU inataka kuweka ukomo kwa bei ya gesi ya Urusi

Rais wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der LeyenPicha: Dursun Aydemir/AA/picture alliance

Suala jengine ambalo limezua maswali mengi hata kuliko majibu ni kuhusu kupanda kwa bei ya nishati kufuatia vikwazo vya nchi za Magharibi kwa Urusi, huku Moscow kwa upande wake ukizuia usafirishaji wa gesi kwenda Ulaya na kuzilaumu nchi za Magharibi kwa kuiwekea vikwazo na pia matatizo ya kiufundi katika mabomba ya kusafirisha gesi.

Wakati Umoja wa Ulaya unapojiandaa kupendekeza ukomo wa bei ya gesi ya Urusi ili kudhibiti mzozo wa nishati ambao unatishia kuenea kwa kasi na kuathiri mataifa ya Ulaya hasa wakati wa msimu wa baridi kali, Putin amejibu kwa kutishia kusitisha kabisa usafirishaji wa gesi iwapo Umoja wa Ulaya utathubutu kuchukua hatua hiyo.

Putin na Scholz wazungumza tena kuhusu Ukraine

01:16

This browser does not support the video element.

Rais wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen amesema, "Tunakabiliwa na hali isiyo ya kawaida, sio tu kwa sababu Urusi ni wasambazaji wasioaminika kama tulivyoshuhudia awali, lakini pia kwa sababu Urusi inajaribu kudhibiti soko la gesi kwa manufaa yao wenyewe."

Bwana Putin amesema Urusi haitosambaza hata chembe ya gesi wala mafuta kwa nchi za Magharibi.

Kwa kawaida, Ulaya huagiza takriban asilimia 40 ya gesi na asilimia 30 ya mafuta yake kutoka Urusi.