1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Putin awaonya Scholz na Macron dhidi ya kuipa silaha Ukraine

28 Mei 2022

Rais wa Urusi Vladimir Putin amewatahadharisha viongozi wa Ujerumani na Ufaransa dhidi ya kupeleka msaada wa silaha nchini Ukraine, akisema hatua hiyo inaweza kuzidisha hali ya ukosefu wa utulivu katika nchi hiyo.

Kombobild Russland Frankreich Putin und Macron
Picha: AFP

Ikulu ya Kremlin imesema Putin amewaambia Rais Emmanuel Macron na Kansela Olaf Sholz kuwa kuendelea kuipatia Ukraine silaha ni "hatari", akionya juu ya hatari ya kuzidisha mzozo wa kibinadamu.

Katika mazungumzo kwa njia ya simu na viongozi hao wawili leo Jumamosi, Putin amesema pia Urusi iko tayari kujadili juu ya njia za kuiwezesha tena Ukraine kusafirisha nafaka kutoka bandari ya bahari nyeusi.

"Kwa upande wake, Urusi iko tayari kusaidia kulitafutia ufumbuzi suala la usafirishaji wa ngano, ikiwa ni pamoja na usafirishaji wa nafaka za Ukraine katika masoko ya nje kutoka bandari ya bahari nyeusi,” Ikulu ya Kremlin imesema.

Soma pia:Wafaransa wapiga kura katika duru ya pili ya urais 

Urusi na Ukraine ni miongoni mwa wauzaji wakubwa wa ngano duniani, wakati Urusi pia ikiwa muuzaji muhimu wa mbolea katika soko la kimataifa. Ukraine inasifika kwa uuzaji wa mahindi na mafuta ya alzeti.

Kremlin imeongeza kuwa, Putin alimjulisha Macron na Scholz kuwa Urusi iko tayari kuongeza mauzo ya nje ya mbolea na bidhaa nyengine za kilimo iwapo tu vikwazo dhidi yake vitaondolewa- ombi ambalo amelitoa katika mazungumzo yake na viongozi wa Italia na Austria katika siku za hivi karibuni.

Scholz na Macron wamtaka Putin kufanya mazungumzo na Zelenksy

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz Picha: Chema Moya/Agencia EFE/IMAGO

Ukraine na mataifa ya Magharibi yameishtumu Urusi kwa kutumia mzozo wa chakula uliosababishwa na uvamizi wake nchini Ukraine kama silaha ya kivita. Mzozo huo umesababisha bei ya bidhaa za vyakula, nafaka, mafuta ya kupikia, na mbolea kupanda maradufu duniani kote.

Hata hivyo, Urusi imezinyooshea kidole cha lawama nchi za Magharibi kwa hali hiyo kutokana na vikwazo ilivyoiwekea Moscow.

Soma pia: Macron, Scholz waepuka kutaja mauaji ya Ukraine kuwa "halaiki"

Kremlin imesema pia kuwa Putin yuko tayari kuanza tena mazungumzo na Ukraine."Hali ya mazungumzo ya amani iligusiwa katika mazungumzo ya leo kati ya Putin na viongozi wa Ufaransa na Ujerumani. Rais Vladimir Putin amethibitisha utayari wa Urusi kuanza tena mazungumzo hayo,” Kremlin imesema.Aidha viongozi hao wa Ujerumani na Ufaransa wamemtaka Rais Putin kufanya mazungumzo ya ana kwa ana na mwenzake wa Ukraine Volodymyr Zelenksy.

Kansela Scholz azungumzia ziara yake Afrika

02:26

This browser does not support the video element.

Ofisi ya Kansela huyo wa Ujerumani imesema, wakati wa mazungumzo kwa njia ya simu yaliyodumu saa moja na dakika 20 kati yao na Putin, viongozi hao wawili wa Umoja wa Ulaya EU walisisitiza juu ya kusitishwa mara moja mapigano na kuondolewa kwa vikosi vya Urusi nchini Ukraine.

Macron na Putin wamemtolea mwito Putin kufanya mazungumzo ya ana kwa ana na Zelenksy na kutafuta suluhusisho la kidiplomasia kwa mzozo huo.

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW