1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Putin awaonya wanaoingilia masuala ya ndani ya Urusi

21 Aprili 2021

Rais wa Urusi, Vladmir Putin amesema baadhi ya nchi zimelifanya suala la kuinyanyasa Urusi kuwa jambo la kawaida na amezionya nchi za Magharibi zinazoingilia masuala ya ndani ya Urusi. 

Russland Moskau | Präsident Putin Rede an die Nation
Picha: EVGENIA NOVOZHENINA/REUTERS

Katika hotuba yake ya kila mwaka kwa bunge na taifa aliyoitoa leo, Rais Putin amezungumzia kuhusu sera ya kigeni ambapo amesema Urusi itachukua hatua kali dhidi ya nchi zinazovuka mipaka.

"Nimelazimika kusema haya. Na tuna uvumilivu wa kutosha, uwajibikaji, taaluma na kujiamini na busara wakati wa kufanya maamuzi yoyote. Nina matumaini kwamba hakuna mtu atakayethubutu kuvuka mstari kwa heshima ya Urusi na tutaamua wapi mstari huo umevukwa kulingana na kila tukio," alifafanua Putin.

Putin: Wachokozi kujutia matendo yao

Katika hotuba hiyo iliyoshuhudiwa na mamia ya wawakilishi wa nyanja za siasa, uchumi na utamaduni, Putin amesema wale wanaopanga uchokozi wowote unaotishia maslahi ya msingi ya usalama wa Urusi, watajuta kwa matendo yao kuliko walivyowahi kushuhudia.

Putin amezungumzia pia kuhusu janga la virusi vya corona pamoja na mageuzi ya mabadiliko ya hali ya hewa na mageuzi ya ndani ya kijamii. Pia ameelezea maendeleo yaliyofikiwa kulifanya jeshi la Urusi kuwa la kisasa.

Hotuba hiyo ameitoa wakati ambapo uhusiano kati ya Urusi na mataifa ya Magharibi ukiwa mashakani kutokana na mzozo wa Ukraine. Jeshi la Urusi limejiimarisha karibu na Ukraine, ambako ukiukaji wa kusitisha mapigano umeshuhudiwa katika mzozo wa miaka saba kati ya waasi wanaoungwa mkono na Urusi na majeshi ya Ukraine.

Mkosoaji wa serikali ya Urusi, Alexei NavalnyPicha: Babuskinsky District Court/AP/dpa/picture alliance

Mzozo huo umeongezeka makali katika wiki za hivi karibuni. Marekani na washirika wake wameitolea wito Urusi kuyaondoa majeshi yake kwenye eneo hilo.

Putin pia amelituhubia taifa wakati ambapo kuna mvutano kuhusu kufungwa jela mkosoaji wake mkuu, Alexei Navalny. Katika pigo kubwa la hivi karibuni la kidiplomasia, Jamhuri ya Czech imeishutumu idara ya usalama ya Urusi kwa kuhusika na shambulizi la mwaka 2014 katika ghala la silaha la Vrbetice.

Vikwazo dhidi ya Urusi

Marekani na Umoja wa Ulaya zimeiwekea Urusi vikwazo kadhaa, huku Marekani pia ikiishutumu nchi hiyo kwa kuhusika na udukuzi wa kimitandao kwenye mashirika ya serikali kuu ya Mrekani.

Marekani, Poland, Bulgaria na Jamhuri ya Czech hivi karibuni ziliwafukuza wanadiplomasia wa Urusi kwa sababu tofauti, na kusababisha Urusi kuchukua hatua ya kulipiza kisasi.

Aidha, Putin amezishutumu nchi za Magharibi kwa kukaa kimya kuhusu jaribio lililoshindwa la kumuua kiongozi wa Belarus, Alexander Lukaschenko. Jaribio hilo lilizimwa na idara za usalama za Belarus, KGB na Urusi FSB. Inaripotiwa kuwa mshukiwa mmoja ni raia wa Marekani.

Kabla ya hotuba hiyo polisi wa Urusi iliwakamata zaidi ya wafuasi 100 wa Navalny na kuzivamia ofisi zake kabla ya maandamano yaliyokuwa yamepangwa kufanyika leo.

 

(DPA, AP, AFP, Reuters)