1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUrusi

Putin aweka rekodi kwenye matokeo ya uchaguzi Urusi

Hawa Bihoga
18 Machi 2024

Rais Vladimir Putin ameshinda kwa kishindo na kuweka rekodi katika uchaguzi wa Urusi uliomalizika siku ya Jumapili, huku akiimarisha madaraka yake. Matokeo ya awali yanaonesha kuwa amepata asilimia 87.8 ya kura.

Matokeo ya kura yakioneshwa katika televisheni
Matokeo ya kura nchini Urusi yakioneshwa katika televisheniPicha: Maxim Shemetov/REUTERS

Akihutubia baada ya kumalizika kwa zoezi la upigaji Kura Putin alisema, matokeo hayo yanapaswa kutuma ujumbe kwa mataifa ya magharibi kwamba viongozi wake watalazimika kuitiambua Urusi yenye ujasiri, iwe ni katika vita ama kwenye amani kwa miaka mingi ijayo.

Kwa matokeo hayo yanayompa ushindi wa kishindo Putin mwenye umri wa miaka 71, anatazamiwa kuanza muhula mpya wa miaka sita utakaomfanya ampiku Josef Stalin na kuwa kiongozi wa muda mrefu zaidi wa Urusi kwa zaidi ya miaka 200 iwapo atamaliza muhula wake.

Putin amepata asilimia 87.8 ya kura, ikiwa hayo ni matokeo ya juu zaidi kuwahi kutokea katika historia ya Urusi baada ya muungano wa Kisovieti kuvunjika. 

Kulingana na kura ya maoni iliyofanywa na mdadisi wa Taasisi ya Maoni ya Umma (FOM). Kituo cha Utafiti wa Maoni ya Umma cha Urusi (VCIOM) kilimuweka Putin kwenye 87%. Matokeo rasmi ya awali yalionyesha kuwa kura zilikuwa sahihi.

Mataifa ya Marekani, Ujerumani, Uingereza na mengine yamesema kuwa uchuguzi huo haukuwa huru na haki kutokana na kufungwa kwa wanasiasa wa upinzani na kudhibitiwa.

Soma pia:Uchaguzi wa rais nchini Urusi kumalizika Jumapili

Mgombea wa Kikomunisti Nikolai Kharitonov ameshika nafasi ya pili kwa kupata chini ya asilimia nne, wakati mgombea wa mara ya kwanza Vladislav Davankov , akishika nafasi ya tatu, huku mwanasiasa wa siasa kali za kizalendo Leonid Slutsky akichukua nafasi ya nne katika matokeo hayo ya awali.

Katika hotuba yake ya ushindi mjini Moscow, Putin amewaambia wafuasi wake kwamba atatoa kipaumbele katika masuala yanayohusiana na kile alichokiita  operesheni maalum ya kijeshi" ya Urusi nchini Ukraine na ataimarisha jeshi la Urusi.

"Tuna majukumu mengi mbele yetu. Lakini tunapojiimarisha bila kujali nani atakayetuyumbisha, kutukandamiza- hakuna aliewahi kufanikiwa katika historia, si kwa sasa na wala si kwa baadae" Putin alisema katika hotuba yake.


Wafuasi wa Navalny waandamana katika vituo vya kura

Maelfu ya wafuasi wa kiongozi wa upinzani Alexei Navalny, aliyefariki katika gereza la Arktik mwezi uliopita wameandamana ndani na nje ya Urusi katika vituo vya kupigia kura dhidi ya rais Putin.

Mjane wa aliekuwa kiongozi wa upinzani aliefia gerezani Alexey Navalny,Yulia Navalnaya akiwa katika kituo cha kupigia kura mjini Berlin UjerumaniPicha: Ebrahim Noroozi/AP/picture alliance

Putin aliwaambia waandishi wa habari kuwa aliuchukulia uchaguzi wa Urusi kuwa wa kidemokrasia na kusema kuwa maandamano yaliyochochewa na afuasi wa Navalny dhidi yake hayakuwa na athari kwa matokeo ya uchaguzi huo.

Katika kauli yake ya kwanza kuhusiana na kifo cha mwanasiasa huyo wa upinzani, Putin alisema kifo cha Navalny kimekuwa "tukio la kusikitisha" na alithibitisha kwamba alikuwa tayari kufanya ubadilishaji wa wafungwa unaohusisha mwanasiasa huyo wa upinzani.

Soma pia:Urusi inafanya uchaguzi katikati ya vita na Ukraine

Hakuna idadi kutoka vyombo huru inayoonesha ni wangapi kati ya wapiga kura milioni 114 wa nchini humo walishiriki katika maandamano ya upinzani, huku kukiwa na ulinzi mkali uliohusisha makumi ya maelfu ya polisi na maafisa wa usalama.

Alipoulizwa na Televisheni ya NBC ya Marekani iwapo kuchaguliwa kwake tena kulikuwa kwa kidemokrasia, Putin alikosoa mifumo ya kisiasa na mahakama ya Marekani.

"Ulimwengu mzima unacheka kile kinachotokea (Marekani)," alisema. "Hili ni janga tu, sio demokrasia."

"Je, ni kidemokrasia kutumia rasilimali za utawala kumshambulia mmoja wa kiti cha urais wa Marekani, kwa kutumia mahakama pamoja na mambo mengine?" aliuliza, akirejelea kesi nne za uhalifu dhidi ya mgombea wa Republican Donald Trump.

Uchaguzi wa Urusi unafanyika ikiwa ni  miaka miwili  tangu Putin aanzishe mzozo mbaya zaidi barani Ulaya tangu Vita vya Pili vya Dunia kwa kuamuru uvamizi kamili kwa jirani yake Ukraine.


Putin aapa kuiadhibu Ukraine kwa kushambulia maeneo yake

Ukraine imefanya mkururo wa mashambulizi katika vituo vya mafuta nchini Urusi, ikiwa ni pamoja na maeneo kadhaa na kutaka kujipenyeza katika mipaka ya Urusi.

Aidha Putin amesema kwamba hatua hiyo haikubaliki na lazima Ukraine iadhibiwe, ameongeza kuwa Urusi inaweza kuunda ukanda salama ndani ya Ukraine ili kuzuia mashambulio kama hayo katika siku zijazo. 

Alisema katika hotuba yake ambayo alitoa salaamu maalumu kwa jeshi la Urusi linaloendesha oparesheni ya kijeshi Ukraine kwamba, vikosi vyake vimeendelea kusonga mbe kwenye uwanja wa vita katika maeneo muhimu Ukraine.

Ujerumani: Hatutaiacha Ukraine kwenye vita peke yake

02:23

This browser does not support the video element.

Soma pia:Warusi wapiga kura katika uchaguzi wa rais utakaodumu hadi Jumapili

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy alisema Jumapili kwamba Putin anataka kutawala milele na kwamba uchaguzi huo haukuwa halali.

Ingawa kuchaguliwa tena kwa Putin hakukuwa na shaka kutokana na udhibiti wake juu ya Urusi na kutokuwepo kwa wapinzani wa kweli, jasusi huyo wa zamani alitaka kuonyesha kwamba anaungwa mkono kwa kiasi kikubwa na Warusi.

Waliojitokeza katika zoezi hilo la kupiga kura nchini kote ni asilimia 74.22 wakati zoezi la upigaji kura lilipofungwa majira ya saa kumi na mbili jioni kwa saa za Urusi, hata hivyo maafisa wa uchaguzi walisema kuwa kiwango hicho kimepiku viwango vya 2018 vilivyokuwa asilimia 67.5


 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW