1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Putin azuru Uturuki kuzungumzia Libya, Syria na gesi

8 Januari 2020

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan leo atakuwa mwenyeji wa mwenzake wa Urusi Vladimir Putin katika hafla ya uzinduzi wa  bomba jipya la gesi huku hofu nchini Libya na Syria pia ikiwa katika agenda ya mazungumzo yao.

Moskau | Vladimir Putin bereitet sich auf die Neujahrsansprache vor
Picha: AFP/M. Klimentyev

Putin aliwasili Uturuki jana jioni baada ya kufanya ziara ya ghafla nchini Syria ikiwa ni ya kwanza nchini humo tangu vita kuzuka wakati wa hali isiyoeleweka katika eneo la Mashariki ya Kati kufuatia mauaji ya jenerali mmoja mkuu wa Iran Qasem Soleimani yaliotekelezwa na Marekani.

Kiongozi huyo wa Urusi atatafuta kuimarisha sifa yake kama mshawishi katika kanda hiyo wakati wa ufunguzi wa bomba hilo la gesi la Turkstream litakalosafirisha gesi ya Urusi hadi Uturuki na Kusini mwa bara Ulaya kupitia bahari nyeusi. Bomba hilo ni moja kati ya mabomba sita yanayofanya kazi ya kusafirisha gesi asilia hadi Uturuki ikiwa ni pamoja na Iran na Azerbaijan. Ujenzi wake ulianza mwezi Mei mwaka 2017.

Mabomba ya gesi ya Turkstream na Nordstream chini ya nchi za eneo la Baltic yanaruhusu Urusi kuongeza usambazaji wa gesi hadi bara Ulaya bila ya kuitegemea Ukraine. Ukraine inatarajiwa kupoteza katika usafirishaji wa gesi ya Urusi kuelekea bara Ulaya pindi bomba la gesi la TurkStream litakapoanza kutumika kikamilifu. Hii ni kulingana na  mtafiti mmoja mkuu katika taasisi ya masomo ya kawi ya Oxford, Julian Bowden.

Uhusiano kati ya Urusi na Uturuki waashiria kuimarika

Lakini kukithiri kwa Urusi katika soko la kawi la bara Ulaya kunaitia hofu Marekani ambayo mwezi uliopita iliiwekea vikwazo kampuni zinazolifanyia kazi bomba la TurkStream na lile linalokaribia kumalizika la Nord Stream 2. Hafla hiyo inayotarajiwa kuanza baadaye nchini Uturuki inaashiria kuimarika kwa uhusiano kati ya Urusi na Uturuki, mataifa mawili yalioonekana kuwa na uwezo wa kuingia katika vita chini ya miaka mitano baada ya Uturuki kulenga ndege ya Urusi.

Mataifa hayo yana misimamo tofauti kuhusiana na mzozo wa Syria na huenda yakazua mgongano nchini Libya.Wiki iliyopita, Uturuki ilituma vikosi vyake vya kwanza kusaidia serikali ya Libya inayoungwa mkono na  Umoja wa Mataifa ambayo imetekwa na mbabe Khalifa Haftar.

Erdogan amesema mamluki 2500 kutoka Urusi ni miongoni mwa wale wanaomuunga mkono Haftar, madai yaliokanushwa naUrusi.Lakini Urusi inaonekana kutobabaishwa na hatua ya kupelekwa kwa vikosi vya kijeshi vya Uturuki nchini Libya. Haya ni kulingana na Mariana Belenkaia wa kituo cha carnegie mjini Moscow. Ameongeza kuwa ''mataifa hayo mawili huenda yakashawishika kugawanya mzigo wa Libya''.

Uhusiano unaozidi kuimarika kati ya mataifa hayo mawili umechochewa na mikataba kadhaa mikubwa ya kawi na ulinzi. Urusi inajenga kiwanda cha kwanza cha kinyuklia cha Uturuki na pia kutengeneza mfumo wa ulinzi wa makombora.Putin pia alijijengea nia njema nchini Uturuki baada ya usaidizi wake wa haraka kwa Erdogan kufuatia majaribio ya kuipindua serikali yake mnamo mwezi Julai mwaka 2016.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW