Putin, Erdogan wakutana kuzungumzia Syria
27 Agosti 2019Mkutano wa viongozi hao mjini Moscow unafanyika siku moja baada ya Erdogan kusema Uturuki iko tayari kutuma majeshi ya ardhini kaskazini mwa Syria, haraka iwezekanavyo ili kuuweka salama mpaka.
Ghasia zinazoongezeka katika jimbo la Idlib zimevuruga makubaliano yaliyofikiwa mwezi Septemba kati ya Urusi na Uturuki ya kutenga eneo lialotenganisha majeshi ya nchi hizo mbili. Msafara wa magari ya jeshi kutoka Uturuki ulishambuliwa katika eneo la kaskazini magharibi mwa Syria juma lililopita licha ya Urusi kutaarifiwa kuhusu msafara huo, wizara ya ulinzi ya Uturuki imesema.
Uturuki wakati huo huo inafanyakazi pamoja na Marekani kutenga eneo litakalokuwa na usalama , karibu na mpaka na Syria , kuwaondoa wapiganaji wa Kikurdi nchini Syria wanaoungwa mkono na Marekani katika eneo hilo na kuzuwia mmiminiko wa wakimbizi wanaoingia Uturuki.
Uturuki inaunga mkono waasi wa upinzani wanaopambana kutaka kumuondoa madarakani rais Bashar al-Asad, ambaye jeshi lake , likiungwa mkono na ndege za kivita za Urusi lilianza mashambulizi dhidi ya waasi jimboni Idlib mwezi wa Aprili.
Majeshi ya Syria
Majeshi ya Syria hivi karibuni kabisa yalichukua tena udhibiti wa mji wa Khan Sheikhoun, mji mkubwa zaidi kusini mwa Idlib, ambao uko katika barabara kuu ya kimataifa inayounganisha Aleppo na Damascus.
Mashambulizi dhidi ya Idlib ni kitisho kwa majeshi ya Uturuki yaliyoko katika vituo vya uangalizi. Uturuki ina vituo 12 vya uangalizi katika jimbo hilo, na licha ya kusongambele kwa majeshi ya Syria, imesema vituo hivyo vyote vitabakia.
Putin na Erdogan walikutana kwanza leo katika ufunguzi wa maonesho ya vyombo vya anga yanayojulikana kama MAKS katika eneo la Moscow, tukio la kila baada ya miaka miwili la viwanda vya kutengeneza ndege.
Rais Vladimir Putin alisema.
"Nafikiri washirika wetu wote wa nje na bila shaka marafiki wetu wa Uturuki, ujumbe wa Uturuki, watahamasika na mafanikio ya viwanda vya ndege vya Urusi pamoja na uwezo wa teknolojia ya jeshi la anga la Urusi katika kizazi cha sasa."
Uturuki mwezi uliopita ilinunua mfumo wa kisasa wa makombora chapa S-400 kutoka Urusi , na kuzusha hasira miongoni mwa wanachama wenzake wa jumuiya ya kujihami ya NATO.