Putin, Erdogan wataka suluhisho la kisiasa Syria
28 Agosti 2019Bado haijafahamika ikiwa pana uhusiano wa kile kilichozungumzwa mjini Moscow hapo jana baina ya Rais Tayyip Erdogan wa Uturuki na mwenyeji wake, Vladimir Putin wa Urusi, na kile kinachoendelea sasa kwenye maeneo mawili tafauti ya Syria.
Lakini ripoti zinasema kuwa mapigano kati ya wanamgambo wanaofungamana na kundi la kigaidi la al-Qaida kusini magharibi mwa Syria walipambana na majeshi ya serikali jioni ya jana, ambapo zaidi ya watu 50 kutoka pande zote mbili waliuawa.
Kwenye mkutano wao mjini Moscow, Erdogan na Putin walielezea wasiwasi wao kuhusu namna hali inavyozidi kuwa mbaya kwenye maeneo kadhaa ya Syria, licha ya makubaliano ya kutoshambuliana baina ya majeshi yao yanayounga mkono pande tafauti kwenye vita hivyo. Rais Putin alisema kiwango cha makabiliano kinatisha, ingawa wanataka kuhakikisha makubaliano ya Astana yanatekelezwa, ukiwemo mpango wa kisiasa kumaliza vita hivyo.
"Kuhusiana na hili, tumejadiliana na Rais Erdogan kuanzisha kamati ya kikatiba, ambayo tunatazamia itaanza kufanya kazi mjini Geneva hivi karibuni," alisema Putin.
Urusi inaunga mkono upande wa serikali, yakiwemo makundi ya Kikurdi yanayopambana dhidi ya wanamgambo wa Dola la Kiislamu, huku Uturuki ikiunga mkono makundi yanayoipinga serikali ya Syria, na wakati huo huo ikipambana na wapiganaji wa Kikurdi inaowachukulia kuwa sehemu ya waasi wa nchini mwake.
Kundi la YPG laondoka mpakani
Kwa upande mwengine, siku moja baada ya mazungumzo ya Putin na Erdogan mjini Moscow, vikosi vya Kikurdi, YPG, vimesema vitaondoka na silaha zake kutoka eneo la mpaka wa Syria na Uturuki, lakini vikitaja makubaliano kati ya Uturuki na Marekani.
Awali ilikuwa imedhaniwa kuwa makubaliano hayo yalikuwa yameingia doa, baada ya Uturuki kukataa shinikizo la Marekani la kutokuagizia mfumo wa kujilinda na makombora kutoka Urusi, na kwenye mazungumzo ya jana, Rais Erdogan alithibitisha kuendelea na mpango huo.
"Tupo kwenye hatua ya pili ya kupokea mfumo huo wa S-400, ambao utaendelea hadi mwishoni mwa mwezi ujao wa Septemba, wakati huu mafunzo kwa watu wetu yanaendelea," alisema rais huyo wa Uturuki.
Msemaji wa kundi hilo mashariki mwa Syria, alisema wanatimiza sehemu ya makubaliano yao ya kuondoka kwenye mpaka wa Tal Abyadh na Al-Ain kwa kuwa wana dhamira ya dhati ya kuendelea na mazungumzo badala ya mapigano.
Kujiondoa huko kunaashiria maendeleo kwenye mazungumzo baina ya Washington na Ankara yenye dhamira ya kutatuwa tafauti zao juu ya kuwepo kwa wapiganaji wa Kikurdi katika eneo hilo la mpaka, ambao Marekani inawachukulia kama msaada kwenye vita dhidi ya Dola la Kiislamu.