Putin kuhudhuria gwaride la ushindi dhidi ya Wanazi
8 Mei 2023Msemaji wa Kremlin, Dmitry Peskov, alisema siku ya Jumatatu (Mei 8) kwamba Rais Putin angekuwepo kwenye gwaride la Jumanne (Mei 9), lakini tayari maafisa wa Moscow walishatangaza kwamba kugelikuwa na kiwango kikubwa kabisa cha ulinzi kwenye maadhimisho hayo ya ushindi wa Wasovieti kwenye Vita vya Pili vya Dunia.
Miji mingine zaidi ya 20 ilifuta maadhimisho hayo ya Siku ya Ushindi kwa sababu ya vitisho dhidi ya usalama wakati huu taifa lao likishiriki uvamizi nchini Ukraine.
Sherehe hizo za Jumane zilitazamiwa kujumuisha tu gwaride la kijeshi kwenye Uwanja Mwekundu, bila ya kuwepo shamrashamra nyengine za kawaida, yakiwemo maonesho ya jeshi la anga.
Soma zaidi:Vita vya Ukraine: Urusi yaishambulia miji ya Kiev na Odessa
Wiki iliyopita, ndege mbili zisizo rubani ziliangukia kwenye ikulu ya Kremlin katika kile ambacho maafisa wa Urusi wanasema ni mashambulizi yaliyofanywa na Ukraine kujaribu kumuua Rais Putin, lakini zikadunguliwa na mfumo wa ulinzi wa anga.
Ukraine imekanusha kuhusika na mashambulizi hayo, na baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kiusalama walidai huenda lilikuwa ni tukio lililofanywa na Urusi yenyewe ili kusaka uhalali wa kampeni yake ya sasa ya mashambulizi mfululizo dhidi ya mji mkuu wa Ukraine, Kiev, na miji mingine.
Von der Leyen kuenda Kiev
Wakati huo huo, Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen, alitazamiwa kuwasili mjini Kiev siku ya Jumanne, kukutana na Rais Volodymyr Zelensky, ikiwa ni mara yake ya tano kuizuru nchi hiyo tangu ivamiwe na Urusi mwezi Februari 2022.
Ziara ya von der Leyen inasadifiana na tarehe 9 Mei, ambayo Umoja wa Ulaya huadhimisha amani ya kudumu baina ya wanachama wake iliyofuatia kumalizika kwa Vita vya Pili vya Dunia mnamo mwaka 1945.
Soma zaidi: Wanajeshi wa Urusi wawahamisha wakazi wa karibu na kinu cha nyuklia cha Zaporizhzhia
Msemaji wa rais huyo wa Kamisheni ya Ulaya alisema von der Leyen angelifanya ziara hiyo kusisitiza juu ya uungaji mkono usio shaka wa Umoja huo kwa wananchi wa Ukraine wanaopambana na uvamizi dhidi yao.
Ziara ya von der Leyen inafanyika wakati Umoja wa Ulaya ukipendekeza duru ya 11 ya vikwazo dhidi ya Urusi ambayo inajumuisha hatua za kuzuia ukwepaji wa vikwazo hivyo, miongoni mwao ikiwa ni kusimamisha usafirishaji wa teknolojia muhimu kwa kampuni nane za Chia zinazotuhumiwa kuziuzia Urusi, kwa mujibu wa waraka ulioonekana na shirika la habari la AFP.
Mabalozi wa Umoja wa Ulaya watakutana siku ya Jumatano kuanza majadiliano juu ya vikwazo hivyo vipya.
Vyanzo: dpa, AFP