Putin na Erdogan kujadili mpango wa usafirishaji nafaka
4 Septemba 2023Putin atampokea Erdogan katika makazi yake yaliyopo kwenye mji wa Sochi na wanatarajia kuzungumzia mkataba huo wa usafirishaji nafaka kupitia Bahari Nyeusi na ambao umekuwa ukisaidia kuepuka uhaba wa chakula duniani hasa katika maeneo ya Afrika, Asia na Mashariki ya Kati.
Mwezi Julai, Putin alikataa kuurefusha mkataba huo ambao ulisimamiwa na Uturuki na Umoja wa Mataifa , akidaia kuwa makubaliano hayo hayakuzingatia ahadi ya kuondoa vikwazo katika mchakato wa mauzo ya nafaka na mbolea za Urusi. Ukraine na Urusi ni wauzaji wakuu wa ngano, shayiri, mafuta ya alizeti na bidhaa zingine muhimu.
Viongozi hao wakitarajia kukutana, Urusi imeendeleza mashambulizi ya ndege zisizo na rubani na kuzilenga sehemu za kusini na katikati mwa Ukraine. Gavana wa kijeshi wa mkoa wa Odessa Oleh Kiper, amesema Ukraine imedungua droni 17 katika wilaya ya Izmail kusini mwa Odessa, lakini kulikuwa na uharibifu mkubwa wa maghala na viwanda vya uzalishaji na vifaa vya kilimo.
Soma pia: Mkataba wa Bahari Nyeusi: Umoja wa Mataifa watuma pendekezo jipya kwa Urusi
Mashambulizi yameripotiwa pia katika eneo la viwanda la Dnipropetrovsk Jumatatu asubuhi. Kwa mujibu wa taarifa za awali, hakukuwa na vifo au majeruhi katika mkoa wa Odessa au huko Dnipropetrovsk. Wanablogu wa kijeshi wa Urusi wameripoti kuwa miundombinu ya bandari katika mlango wa ziwa Danube ilishambuliwa tena katika mkoa wa Odessa.
Ukraine yadai kupata mafanikio eneo la kusini
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema siku ya Jumatatu kuwa vikosi vyake vimepata mafanikio dhidi ya vikosi vya Urusi katika eneo la mashariki na kwamba wamefanikiwa kuchukua tena udhibiti wa kilometa tatu za mraba karibu na mkoa wa Bakhmut.
Naibu Waziri wa Ulinzi Ganna Malyar amesema Urusi inapambana kuilinda mikoa ya Zaporizhzhia na Kherson, ambayo Moscow ilidai kuinyakua mwaka jana. Malyar amesema Urusi inapata hasara kubwa ya watu na vifaa katika eneo la kusini.
Siku ya Jumapili, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alitangaza mabadiliko katika wizara ya ulinzi na hii leo Waziri Oleksiy Reznikov aliyekuwa akishikilia wadhifa huo ametangaza kuwa amewasilisha barua yake ya kujiuzulu kwa Bunge baada ya Zelensky kutoa wito wa kile alichokitaja kuwa "mbinu mpya" katika kukabiliana na uvamizi wa Urusi.
Uamuzi wa Zelensky wa kumuondoa Reznikov unajiri baada ya kashfa kadhaa za ufisadi kuitikisa wizara ya ulinzi, na kiongozi huyo wa Ukraine amewafuta pia kazi maafisa wakuu kote nchini humo wanaohusika na usajili jeshini.
Katika mkutano wa nchi 20 zilizostawi kiviwanda na zinazoinukia kiuchumi (G20) unaotarajiwa mwishoni mwa jumaa hili mjini New Delhi nchini India, uvamizi wa Urusi nchini Ukraine huenda ukawa kizingiti kwa masuala mengine muhimu kama usalama wa chakula duniani, tatizo la madeni kimataifa na ushirikiano juu ya mabadiliko ya tabia nchi.