Putin kukutana na Macron mjini Paris
29 Mei 2017Baada ya Moscow kupoteza utabiri wake katika kura ya Ufaransa, ziara hiyo inampatia nafasi kiongozi wa Urusi kuweza kuugeza ukurasa na kuanzisha mahusiano na Macron wakati Ikulu ya Kremlin ikijitahidi kurekebisha nyufa zilizojitokeza baina yake na mataifa ya magharibi.
Mkutano huo unakuja baada ya kumalizika kwa mkutano wa kilele wa nchi saba zenye nguvu duniani mwishoni mwa juma ambapo mahusiano na Urusi yalikuwa ni sehemu ya ajenda za mkutano huo, na kumfanya Macron kuwa kiongozi wa kwanza wa Magharibi kuzungumza na Putin.
Ikulu ya Kremlin imesifu ziara hiyo ikisema ni fursa ya kipekee kwa Putin na Macron kufahamiana vyema na kupata uelewa mzuri juu ya mitazamo yao kuhusu migogoro kadhaa, ikiwemo mgogoro wa Ukraine, vita nchini Syria na mahusiano ya Urusi na Umoja wa Ulaya.
Mwaliko wa Macron kwa Putin umekuja kwa mshangao baada ya msimamo wake mgumu kwa Urusi wakati wa kampeni za urais ambao ulitofautiana na ule wa wapinzani wake akiwemo mgombea wa siasa kali za mrengo wa kulia Marine Le Pen na mhafidhina Francois Fillon ambao wote walisema wangeondoa vikwazo vya nchi za magharibi dhidi ya Moscow kuhusu mgogoro wa Ukraine.
Katikati mwa uchunguzi wa bunge na ule wa Shirika la upelelezi la Marekani FBI juu ya madai ya Urusi kuingilia kati uchaguzi wa rais wa nchi hiyo, wasaidizi wa Macron walidai kwamba mnamo mwezi Februari makundi ya Urusi yaliingilia kati kampeni zake. Moscow iliyakana vikali madai hayo ya kuingilia kati chaguzi.
Putin, hata hivyo alibainisha wazi nani ni chaguo lake katika uchaguzi wa Ufaransa baada ya kumualika Le Pen mnano mwezi machi ikiwa ni sehemu ya jitihada za Urusi za kuwafikia wanasiasa wenye misimamo ya kizalendo na kundi la wale wanaopinga utandawazi kwa matumaini ya kuongeza ushawashi wao kwa mataifa ya magharibi.
Kwa miaka kadhaa, Putin amekuwa akikutana na Fillon, waziri mkuu wa Ufaransa kati ya mwaka 2007-2012 na kumsifu kuwa ni mtu aliye na uzoefu mkubwa wa masuala ya kitaifa.
Wachambuzi wanasema ziara hiyo itampatia fursa Rais Putin ya kuboresha mahusiano yake na Ufaransa ambayo yalikuwa yameporomoka katika miezi ya mwishoni ya rais Francois Hollande.
Mnamo mwezi Oktoba, Putin alifuta ziara yake mjini Paris baada ya Hollande kusema kwamba Urusi inaweza kukabiliwa na makosa ya uhalifu wa vita kuhusu Syria. Hollande alitangaza kwamba asingeweza kushiriki katika ufunguzi wa kituo cha Urusi cha utamaduni na kiroho cha madhehebu ya Orthodox kilichofunguliwa mjini Paris na kusema alichotaka ni mazungumzo tu na Putin kuhusu Syria.
Putin na Macron watafanya mazungumzo yao Versailles na kisha kuhudhuria sherehe ya kumbukumbu ya miaka 300 ya ziara ya Mfalme Peter wa Urusi mjini Paris, sherehe ambayo imeandaliwa na makumbusho ya turathi ya mji wa St. Petersburg.
Mwandishi: Sylvia Mwehozi/AP
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman