Putin kusaini makubaliano ya ushirikiano na Korea Kaskazini
18 Juni 2024Katika barua iliyochapishwa na vyombo vya habari vya serikali ya Korea Kaskazini kuelekea ziara yake nchini humo, Putin pia ameiahidi Pyongyang msaada usio na shaka.
Kiongozi huyo wa Urusi amesema nchi hizo mbili zimeimarisha uhusiano mzuri katika kipindi cha miaka 70, uliobuniwa kwa misingi ya usawa, kuheshimiana na uaminifu.
Soma pia: Korea Kaskazini yakanusha kubadilishana silaha na Urusi
Putin ameishukuru Korea Kaskazini kwa kuiunga mkono Urusi katika "oparesheni yake maalum ya kijeshi" nchini Ukraine.
Barua hiyo imechapishwa siku moja baada ya nchi hizo mbili kutangaza kuwa Putin ataitembelea Korea Kaskazini kwa mara ya kwanza katika muda wa miaka 24 kuanzia leo Jumanne.
Mshauri wa sera za kigeni wa Putin Yuri Ushakov amesema Urusi na Korea Kaskazini huenda zikatia saini makubaliano ya ushirikiano wakati wa ziara hiyo yatakayojumuisha masuala ya usalama.