1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Putin kusaini mikataba ya ushirikiano mjini Pyongyang

Sylvia Mwehozi
18 Juni 2024

Rais wa Urusi Vladimir Putin anaelekea nchini Korea Kaskazini katika ziara yake ya kwanza ndani ya kipindi cha miaka 24. Kiongozi huyo anaitembelea nchi hiyo iliyotengwa kimataifa.

Putin-Moscow
Rais wa Urusi Vladimir PutinPicha: Valentina Pevtsova/Pool Sputnik Kremlin via AP/dpa/picture alliance

Kiongozi huyo wa Urusi na mwenzake wa Korea Kaskazini wanatarajiwa kusaini mkataba wa ushirikiano thabiti wakati wa ziara ya Putin mjini Pyongyang. Putin anaitembelea Korea Kaskazini ambayo imetengwa katika kile ambacho maafisa wamekitaja kuwa ni "ziara rafiki ya kitaifa".

Rais Putin ameidhinisha rasimu ya mkataba ulioandaliwa na wizara ya mambo ya nje ya Urusi. Mkataba huo utasainiwa na Putin mwenyewe na Kim. Hakuna maelezo yaliyotolewa kuhusu undani wa mkataba huo.

Kabla ya kutua Pyongyang, Putin alizuru mkoa wa Urusi wa Yakutsk na ataondoka nchini Korea Kaskazini siku ya Jumatano akielekea Vietnam. Kuelekea ziara yake, Putin  ameimwagia sifa Korea Kaskazinikwa "uungwaji wake mkono usioyumba kwa jeshi la Urisi katika operesheni yake nchini Ukraine", katika barua iliyochapishwa kwenye gazeti la Korea la Rodong Sinmun.

Rais wa Urusi Vladimir Putin alipompokea kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un 2023Picha: Vladimir Smirnov/AFP

Kiongozi huyo wa Urusi pia ameishukuru Korea Kaskazini kwa mshikamano wake juu ya masuala muhimu ya kimataifa, akiongeza kuwa "ilikuwa inajitolea na yenye kujitambua" tayari kukabiliana na matarajio ya nchi za magharibi ya kuzuia uanzishwaji wa mpangilio wa usawa wa dunia kutokea pande tofauti.

Kulingana na Putin, nchi zote mbili zina mipango ya kushirkiana katika kuunda muundo wa kiusalama katika kanda ya Ulaya na Asia na kukabiliana na vikwazo vya Magharibi sambamba na kuanzisha mfumo huru wa miamala ya fedha. Kim ausifu uhusiano unaotanuka wa Korea Kaskazini na Urusi

Kiongozi huyo wa Urusi alipokea mwaliko kutoka kwa Kim kwa mazungumzo mjini Pyongyang juu ya kuimarisha ushirkiano wa kijeshi na masuala mengine, kwa mujibu wa ikulu ya Urusi ya Kremlin. Aidha pia Rais Putin ameapa kuiunga mkono Pyongyang dhidi ya Marekani wakati wa ziara yake nchini humo ambayo ni ya kwanza kuifanya ndani ya miaka 24.

Rais wa Urusi Vladimir Putin alipompokea kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un 2023Picha: Shamil Zhumatov/Pool Photo/AP Photo/picture alliance

Soma: Putin kufanya ziara ya nadra ya siku mbili Korea Kaskazini

Uhusiano wa karibu na wa muda mrefu kati ya Korea Kaskazini na Urusi unatizamwa kwa mashaka na Marekani na washirika wake. Kwa mujibu wa nchi za Magharibi, Korea Kaskazini inaipatia Urusi silaha katika vita vyake nchini Ukraine. Wasiwasi huo umegusiwa na katibu mkuu wa jumuiya ya kujihami NATO Jens Stoltenberg. 

"Urusi sasa inashirikiana zaidi na zaidi na viongozi wa kimabavu, Iran, Beijing, lakini pia na Korea Kaskazini. Na Korea Kaskazini ilisambaza zaidi ya silaha milioni moja za kivita kwa Urusi. Kwa hiyo Korea Kaskazini inaisaidia Urusi kuendesha vita vya kichokozi dhidi ya Ukraine. Na  Urusi inatoa ujuzi wa teknolojia kwa ajili ya programu zao za makombora na nyuklia."

Korea Kaskazini ni nchi iliyotengwa kimataifa huku ikikabiliwa na vikwazo vizito kutokana na mpango wake wa silaha za nyuklia. Mnamo Septemba mwaka 2023, Kim aliizuru Urusi katika ziara ya nadra nje ya nchi na kuungana na mwenyeji wake Putin.