Putin kuzungumza na Erdogan
28 Juni 2016Kwa mujibu wa msemaji wa ikulu ya Urusi Kremlin, hii itakuwa mara ya kwanza kwa viongozi hao kuzungumza baada ya rais Erdogan kumtumia ujumbe Putin wa kuiomba radhi familia ya rubani aliyeuawa na kuonyesha utayari wa kujenga tena mahusiano baina yake na Urusi.
Rais Vladimir Putin amesema msamaha huo kutoka kwa Erdogan ulikuwa ni sharti kwa ajili ya kuyarejesha mahusiano baina ya nchi hizo mbili yaliyovunjika kufuatia ndege ya Urusi kudunguliwa mpakani mwa Syria na Uturuki.
Dmitry Peskov msemaji wa Kremlin amesema kwamba na hapa namnukuu, "rais Putin ameelezea zaidi ya mara moja kuwa yupo tayari kurejesha uhusiano na Uturuki na watu wake, na sasa hatua kubwa imepigwa" mwisho wa kumnukuu.
Vita ya Syria
Urusi na Uturuki zimekuwa zikizozana juu ya vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria, ambako zinaunga mkono makundi pinzani. Urusi imekuwa na kampeni ya urushwaji wa mabomu ya kuiunga mkono serikali ya Syria inayopigana kurejesha utulivu katika nchi.
Wakati huo huo, Uturuki yenyewe inalisaidia kundi la waasi linapigana kuiondoa serikali madarakani , inayoshutumiwa kwa uhalifu dhidi ya ubinadamu, ikiwemo mauaji ya raia.
Urusi iliiyoiwekea vikwazo vya kiuchumi Uturuki kutokana na mkasa huo, imesema pamoja na kuomba radhi lakini pia inaitaka Uturuki kulipa fidia ya tukio hilo. Hata hivyo waziri mkuu wa Uturuki Binali Yildirim amesema hii leo kwamba Uturuki haiko tayari kutoa fidia kwa Urusi kwa kuidungua ndege hiyo. Amewaambia waandishi wa habari bungeni kuwa, "mawasiliano baina ya viongozi wawili Tayyip Erdogan na Vladmir Putin ambayo yalikuwa yakiendelea , hatimaye yamepata majibu. Inaonekana kwamba kuna maelewano ya kujenga uhusiano kati ya Urusi na Uturuki. Kwa hiyo tunaweza sema mchakato wa kuyarejesha umeanza."
Ameongeza kwamba hatua za kisheria zitatumika dhidi ya mtu aliyeidungua ndege na kumuua rubani wa urusi.
Majeshi ya Uturuki yaliidungua ndege ya Urusi, yakidai kwamba iliingilia anga la Uturuki, miezi miwili baada ya Urusi kuanza kampeni zake za kijeshi za kuisaidia Syria. Urusi ilikataa madai ya kwamba ndege yake hiyo iliingia katika anga la Uturuki.
Mwandishi: Sylvia Mwehozi/DPA/Reuters
Mhariri: Mohammed Khelef