1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUlaya

Putin: Mashambulizi ya Ukraine hayatazima oparesheni yetu

Hawa Bihoga
12 Agosti 2024

Rais wa Urusi Vladimir Putin amesema uvamizi wa jeshi la Ukraine katika eneo la Kursk ambalo limesababisha madhara, ni jaribio la Kyiv kuzuia mashambulizi ya Moscow katika eneo la mashariki mwa Ukraine.

Urusi | Rais Vladimir Putin akiwa na watendaji wake wa ulinzi na usalama.
Rais wa Urusi Vladimir Putin akiwana na Waziri wake wa Ulinzi Andrei Belousov na Mkuu wa kikosi cha wanamaji Admiral Alexander Moiseyev.Picha: Dmitri Lovetsky/REUTERS

Vikosi vya Urusi bado vinajitahidi kujibu mashambulizi ya kushtukiza ya Ukraine baada ya takriban juma moja la mapigano makali, lakini rais Putin anasisiza kuwa jeshi lake litashinda.

Akizungumza katika mkutano na maafisa wa ngazi za juu wa usalama na ulinzi, rais Putin amesema mashambulizi yalioanza Agosti 6 yanaonekana kuakisi jaribio la Kyiv la kupata nafasi nzuri katika mazungumzo yanayoweza kumaliza vita.

Katika mkutano huo alisema Ukraine inaweza kuwa na matumaini ya kuteteresha hali na kusababisha machafuko nchini Urusi kufuatia mashambulizi hayo lakini lengo hilo halitatimia, na kuongeza kwamba jeshi lake limezidi kuimarika kwani kuna idadi kubwa ya watu waliojitolea kujiunga na jeshi na kwamba vikosi vya urusi vinaendeleza mashambulizi mashariki mwa Ukraine.

Soma pia:Putin aamuru jeshi kuwang'oa mpakani askari wa Ukraine

Gavana wa eneo la Urusi ambalo kwa sasa linashuhudia mashambulizi makali ya Ukraine la Kursk Alexei Smirnov amemwambia rais Putin kwamba, vikosi vya Ukraine vimesonga mbele katika eneo hilo na kwa sasa vinadhibiti makaazi 28 ya Warusi, Smirnov ameongeza kwamba katika oparesheni hiyo takriban raia 12 wameuwawa na wengine 121 wamejeruhiwa wakiwemo watoto 10.

Kiasi cha watu 121,000 wamehamishwa ama kuyakimbia maeneo hayo ambayo yameathiriwa na mapigano kwa takriban juma moja sasa. Kufuatia hali tete katika eneo hilo

Rais Putin amesema ni "dhahiri kwanini utawala wa kyiv ulikataa mapendekezo yetu ya kurejea kwenye mpango wa amani, kadhalika mapendekezo ya wapatanishi wenye nia na wasioegemea upande wowote."

Rais Putin aliongeza kwamba "inavyoonekana, adui kwa msaada na washirika wake wa magharibi wanatimiza malengo yao, na mataifa ya Magharibi yanapigana nasi kupitia Ukraine."

Ukraine inatumia silaha za NATO kushambulia Urusi?

Mapigano ndani ya Urusi yamezuwa maswali mengi kuwa iwapo Ukraine imetumia silaha zilizotolewa na wanachama wa NATO katika mashambulizi yake ya hivi karibu.

Baadhi ya mataifa ya Magharibi yamegoma kuiruhusu Ukraine kutumia misaada yao ya kijeshi kushambulia ndani ya Urusi, wakihofia kwamba ingelichochea mzozo zaidi ambao unaweza kuitumbukiza Urusi na NATO kwenye vita.

Mashambulizi ya Urusi yameua zaidi ya watu 30 Ukraine

02:10

This browser does not support the video element.

Ingawaje haijulikani ni silaha gani Ukraine inatumia kushambulia maeneo hayo ya mpakani, vyombo vya habari vya Urusi vimeripoti kwamba magari ya kivita ya Marekani na Ujerumani yalionekana kwenye uwanja wa vita, madai ambayo hayakuweza kuthibitishwa kwa mizani sawia.

Soma pia:Zelenskiy kulihutubia bunge la Marekani

Ndani ya Ukraine Rais Volodymyr Zelensky amesema bado wanauhitaji wa mifumo thabiti ya anga kutoka kwa washirika wake wa magharibi katika wakati ambako kunashuhudiwa mashambulizi ya vikosi vya Urusi hasa katika maeneo ya Donbas.

Aliongeza kwamba lipo hitaji la kufunga anga la Ukraine kwa mashambulizi ya droni pamoja na makombora ya Korea Kaskazini ambayo amedai urusi inayatumia.

Akizungumzia mashambulizi ya hivi karibuni alisema kwamba, Urusi ilianzisha takriban mashambulizi 2,000 ya kuvuka mpaka kutoka eneo lake la magharibi la Kursk  jambo ambalo alisema lilistahili jibu "la haki" kutoka Ukraine.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW