Putin, Modi, viongozi wengine wako China kwa mkutano wa SCO
31 Agosti 2025
Mkutano wa kilele wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai (SCO) umeanza mjini Tianjin, kaskazini mwa China, ukiwaleta pamoja viongozi kutoka zaidi ya nchi 20. Huu ndiyo mkutano mkubwa zaidi tangu kuanzishwa kwa jumuiya hiyo mwaka 2001, na unafanyika siku chache kabla ya gwaride kubwa la kijeshi jijini Beijing kuadhimisha miaka 80 tangu kumalizika kwa Vita Kuu ya Pili ya Dunia.
Rais Xi Jinping na Waziri Mkuu wa India Narendra Modi walikutana kwa mazungumzo ya pande mbili katika tukio linaloashiria mwanzo mpya ya kidiplomasia kati ya mataifa hayo mawili yenye idadi kubwa zaidi ya watu duniani. Modi alisema India imejitolea "kuendeleza mahusiano kwa heshima, uaminifu na uelewano,” huku Xi akisisitiza kuwa China na India "ni washirika, si wapinzani.”
Mambo ya msingi ya mkutano
Jumuiya ya SCO kwa sasa inaundwa na China, India, Urusi, Pakistan, Iran, Kazakhstan, Kyrgyzstan, Tajikistan, Uzbekistan na Belarus, huku nchi 16 nyingine zikishiriki kama waangalizi au washirika wa mazungumzo. Rais wa Urusi Vladimir Putin, Rais wa Iran Masoud Pezeshkian, na Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan wamo miongoni mwa viongozi wanaohudhuria.
Kwenye mitaa ya Tianjin, mabango makubwa yenye ujumbe wa "ushirikiano wa faida kwa wote” na "usawa” yamepandishwa, wakati polisi na vikosi vya usalama vikidhibiti maeneo makuu ya jiji hilo.
Diplomasia ya Xi na Modi
Ziara hii ya Modi ni ya kwanza nchini China tangu mwaka 2018 na inakuja baada ya Marekani kuweka ushuru wa asilimia 50 kwenye bidhaa za India kama adhabu kwa ununuzi wake wa mafuta kutoka Urusi. Wachambuzi wanasema hali hii imekuwa kichocheo cha India na China kutafuta mbinu mpya za ushirikiano wa kiuchumi na kisiasa.
Mazungumzo hayo pia yamefungua ukurasa mpya katika kusuluhisha mzozo wa mpaka uliosababisha mapigano ya mwaka 2020 na kuua wanajeshi 24. Pande zote mbili sasa zimekubaliana kuimarisha utulivu mpakani na kurejesha safari za moja kwa moja na visa za watalii.
Ushirikiano wa kieneo na changamoto
China na Urusi zimekuwa zikilitumia jukwaa la SCO kama mbadala wa muungano wa NATO, na mkutano huu unachukuliwa kama jukwaa la kuimarisha ushawishi wa nchi zisizo za Magharibi. Putin anatarajiwa kufanya mazungumzo na Erdogan kuhusu mzozo wa Ukraine, huku akikutana na viongozi wa Iran kujadili mpango wa nyuklia.
Hata hivyo, wachambuzi wanabashiri kuwa India haitageuka kabisa kuikabili Magharibi kwa sababu ya maslahi yake ya kiusalama, ikizingatia nafasi yake kwenye ushirikiano wa usalama wa Indo-Pacific maarufu kama Quad unaoshirikisha pia Marekani, Japan na Australia.
Maangamizi na matarajio
Licha ya matumaini ya kuimarisha urafiki, changamoto bado zipo, ikiwemo pengo kubwa la kibiashara kati ya China na India, mradi wa bwawa kubwa la China Tibet unaohatarisha upatikanaji wa maji nchini India, na uhusiano wa karibu wa China na Pakistan – mpinzani mkubwa wa India.
Hata hivyo, wachambuzi wanasema hatua hii mpya ya kujongeleana kati ya Beijing na New Delhi inaweza kuwa hatua muhimu kuelekea usawa mpya wa mahusiano, hasa katika wakati ambapo dunia inakabiliana na ushindani mkali kati ya kambi za Mashariki na Magharibi.
Chanzo: dpae, rtre,afpe