1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Putin na Lukashenko wafanya mazungumzo Urusi

23 Julai 2023

Rais wa Urusi Vladimir Putin amefanya mazungumzo na mwenzake wa Belarus Alexander Lukashenko leo Jumapili. Viongozi hao wawili wamekutana mjini St. Petersburg.

Rais Vladmir Putin na Alexander Lukaschenko mjini St. Petersburg
Rais Vladmir Putin na Alexander Lukaschenko mjini St. PetersburgPicha: Alexander Demianchuk/TASS/dpa/picture alliance

Awali katika mazungumzo yao, Putin alisema mashambulizi ya Ukraine kwa Urusi yamekwama. Video iliyochapishwa mapema leo na kitengo cha habari cha Lukashenko iliwaonesha viongozi hao wakiwasili katika kasri la Konstantinovsky la mjini St. Petersburg kabla ya mazungumzo yao kuanza.

Kwenye mazungumzo hayo, yatakayodumu kwa muda wa siku mbili, wawili hao watazungumzia masuala ya usalama mashariki mwa Ulaya. Haya ni mazungumzo ya kwanza ya ana kwa ana kati ya Putin na Lukashenko, tangu Belarus ilipoisaidia kusimamisha uasi wa kundi la Wagner nchini Urusi.

Urusi na Belarus ni washirika wa muda mrefu katika uhusiano ambao Moscow ndiyo inayotawala sehemu kubwa ya ushirika huo. Hata hivyo Lukashenko amekuwa akionesha umuhimu wake kwa Putin tangu majeshi ya Urusi yalipoivamia Ukraine Februari 2022 ambapo aliruhusu Belarus itumike kama sehemu ya kufanikisha mashambulizi mwanzoni mwa vita.

Rais wa Belarus Alexander Lukashenko Picha: Alexander Zemlianichenko/AP/picture alliance

Aliruhusu majeshi ya Moscow yafanye mafunzo katika ngome zake za kijeshi. Mafunzo hayo mara nyingi yalihusisha mazoezi ya pamoja ya kijeshi na alipokea silaha za kimkakati za nyuklia ambazo Putin amezipeleka Belarus, hatua iliyolaaniwa vikali na mataifa ya magharibi.

Ikulu ya Kremlin ilimpongeza pia Lukashenko kwa kusimamia makubaliano ya mwezi uliopita ya kuzima uasi wa wapiganaji wa Wagner ambao Putin anasema kwa muda mfupi, ulitishia kuiingiza Urusi katika vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Lukashenko hajatoa ahadi ya kupeleka jeshi lake dogo liungane na Moscow katika vita, lakini hatari ya mashambulizi mapya kutoka katika ardhi ya Belarus inaisukuma Ukraine kulinda mpaka wake wa upande wa kaskazini.

Mashambulizi dhidi ya Ukraine yaendelea, Odessa yashambuliwa tena

Katika hatua nyingine, Urusi imeushambulia tena mji wa bandari ya Bahari Nyeusi wa Odesa nchini Ukraine. Taarifa hiyo imetolewa na maafisa wa Ukraine wakati Urusi ikiendeleza mashambulizi ambayo yameharibu miundo mbinu muhimu ya bandari kusini mwa Ukraine katika wiki moja iliyopita.

Soma zaidi: Watu kadhaa wameuawa na wengine kujeruhiwa katika mji wa bandari wa Odessa nchini Ukraine

Muonekano wa sehemu ya uharibifu uliotokana na mashambulizi mjini OdessaPicha: Nina Liashonok/REUTERS

Mashambulizi hayo yamesababisha kifo cha mtu mmoja, watu wengine 22 wamejeruhiwa kwenye tukio hilo lililosambaratisha pia kanisa ambalo ni alama muhimu ya dhehebu la Orthodox kwenye mji huo.

Gavana wa eneo hilo Oleh Kiper amesema, watoto wanne ni kati ya waliojeruhiwa katika mlipuko uliotokana na shambulio hilo. Kiper ameeleza kuwa, majengo sita ya makazi ya watu nayo yameharibiwa.

Urusi imekuwa ikifanya mashambulizi mfululizo kuilenga Odesa, mji ambao ni kituo muhimu cha kusafirisha nafaka tangu Moscow ilipojitoa katika mkataba wa usafirishaji wa bidhaa za kilimo Jumatatu licha ya juhudi za Kyiv kutaka kurejesha maeneo yake yaliyonyakuliwa na Urusi.