1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Putin na Xi wahudhuria mkutano wa kilele wa SCO huko Astana

4 Julai 2024

Rais wa Urusi Vladimir Putin na yule wa China Xi Jinping wamehudhuria siku ya Alhamisi mkutano wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Shanghai SCO iliyoundwa na madola hayo mawili ili kukabiliana na miungano ya nchi za Magharibi.

Viongozi wa SCO wakiwa wamekusanyika mjini Astana, Kazakhstan
Viongozi wa SCO wakiwa wamekusanyika mjini Astana, Kazakhstan: 04.07.2024Picha: Sergei Savostyanov/Tass/dpa/picture alliance

Mkutano huo unaofanyika Kazakhstan, jumuiya ya SCO pia imemkaribisha mwanachama mpya ambayo ni Belarus na kuahidi kuimarisha mahusiano yao ya kiuchumi na kiusalama.

Putin na Xi waliungana na viongozi wa nchi zingine ambazo ni wanachama wa Jumuiya hiyo ya Ushirikiano ya Shanghai katika mkutano wao wa kila mwaka ambao mara hii unafanyika katika mji mkuu wa Kazakhstan, Astana.

Akihutubia mkutano huo, Putin amesisitiza umuhimu kwa kundi hilo katika kuhakikisha usalama wa nchi wanachama na kwamba SCO itaunda kituo ambacho kitaratibu mikakati ya kukabiliana na changamoto mbalimbali za kiusalama. Rais huyo wa Urusi ameongeza kuwa wanachama wa kundi hilo wanatazamiwa kuunga mkono mpango maalumu wa kupambana na itikadi kali na zile zinazosababisha mfarakano.

Soma pia: Putin na Xi watazamia kuongeza ushawishi katika mkutano wa kilele Kazakhstan

Kwa upande wake Xi Jinping amewatolea wito wanachama wa SCO kujihadhari na uingiliaji wa kigeni, kuonyesha mshikamano wa dhati dhidi ya changamoto mbalimbali na kusisitiza umuhimu wa kulinda misingi ya usalama hasa katika nyakati hizi za kukabiliana na tishio la fikra juu ya uwezakano wa kuzuka kwa Vita Baridi.

Kuimarika kwa mahusiano kati ya Urusi na China

Urusi na China wadhihirisha kuimarika kwa mahusiano yao, kama alivyosisitiza rais Putin:

Rais wa Urusi Vladimir Putin (kulia) akisalimiana na Rais wa China Xi Jinping pambezoni mwa mkutano huo wa SCO huko Astana: 03.07.2024Picha: Sergey Guneyev/Pool Sputnik Kremlin/AP/picture alliance

"Tumeeleza zaidi ya mara moja kwamba ushirikiano wa kimkakati wa pande mbili kati ya Urusi na China kwa ajili ya zama mpya, uko katika kipindi bora zaidi kihistoria. Uhusiano kati ya Urusi na China umejengeka katika misingi ya usawa, kunufaishana na kuheshimu uhuru wa kila mmoja wetu. Ushirikiano wetu haumlengi yeyote, wala hatujaunda kambi au muungano wowote. Sisi tunafanya kazi kwa dhamira ya kutetea maslahi ya watu wetu. "

Soma pia: Putin asifu uhusiano imara kati ya Urusi na China

Aidha Putin amesema pia kuwa wanaunga mkono ombi la Iran:

"Nchi wanachama wa shirika (SCO) wanazingatia ombi la Iran la kupata hadhi ya kuwa nchi mwangalizi katika Jumuiya ya Kiuchumi na kiusalama. Sisi kwa upande wetu tunaunga mkono hili."

Kando na  Putin, Xi  na mwenyeji wa mkutano huo wa wa kilele Rais wa Kazakhstan Kassym-Jomart Tokayev, viongozi wengine wanaohudhuria mkutano huo ni Waziri Mkuu Shehbaz Sharif wa Pakistan, Rais Shavkat Mirziyoyev wa Uzbekistan, Rais Emomali Rakhmon wa Tajikistan, Rais Sadyr Zhaparov wa Kyrgyzstan na Rais Alexander Lukashenko wa Belarus. Waziri Mkuu Narendra Modi wa India amewakilishwa na waziri wake wa mambo ya nje.

Historia fupi ya Jumuiya hiyo ya SCO

Mwenyeji wa mkutano huo Rais wa Kazakhstan Kassym-Jomart Tokayev akihutubia mkutano huo wa SCO mjini AstanaPicha: Turar Kazangapov/REUTERS

Jumuiya ya SCO ilianzishwa kwa pamoja na China na Urusi mnamo mwaka 2001 na kuyajumuisha mataifa manne ya Asia ya Kati yaliyokuwa sehemu ya uliokuwa Muungano wa Kisovieti ambayo ni Kazakhstan, Kyrgyzstan, Tajikistan na Uzbekistan. Baadaye mataifa ya India, Pakistan na Iran yalijiunga.

Soma pia: Belarus yajiunga na Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai

Lengo kuu ilikuwa  kuimarisha usalama wa kikanda na kudumisha ushirikiano wa kiuchumi na shirika hilo la kiusalama linachukuliwa kama chombo muhimu cha kuendeleza malengo ya kimkakati ya nchi wanachama katika kanda ya Ulaya na Asia.

siku ya Alhamisi, Belarus ambayo ni mshirika wa karibu wa Urusi imejiunga rasmi na Jumuiya hiyo ya Ushirikiano ya Shanghai (SCO), na kuwa mwanachama wa kumi wa kundi hilo. Mataifa waangalizi na washirika  wa muungano huo ni pamoja na Uturuki, Saudi Arabia na Misri.

(Vyanzo: Mashirika)

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW