1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUrusi

Putin: Urusi iko tayari kwa mazungumzo.

5 Januari 2023

Rais wa Urusi Vladimir Putin amemueleza mwenzake wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan hii leo kwamba Urusi iko tayari kwa mazungumzo kuhusiana na suala la vita vya Ukraine.

Erdogan und Putin (Archivbild)
Picha: Mikhail Metzel/ITAR-TASS/IMAGO

Rais wa Urusi Vladimir Putin hata hivyo amesema hayo yanawezekana ikiwa Kyiv itatimiza sharti la kukubali kuyaachia maeneo yake yaliyonyakuliwa na Urusi. Amesema hayo, alipozungumza na Erdogan, ambaye ameongeza shinikizo kwa Putin la kusitisha mapigano. 

Soma Zaidi: Ukraine yataja masharti ya kufanya mazungumzo na Moscow

Sehemu ya taarifa iliyochapishwa na ikulu ya Kremlin imesema Vladimir Putin amerudia tena matamshi yake kwamba yuko tayari kwa mazungumzo thabiti, kwa kuzingatia tu kwamba Kyiv itatekeleza masharti yaliyojulikana na kurudiwa mara kwa mara ya kukubali kuyaachia maeneo hayo.

Jenerali wa Urusi asema Moscow inalenga kudhibiti maeneo yote ya kusini mwa Ukraine

Mapema, rais Erdogan aliongeza shinikizo kwa Putin akimtaka kusitisha mapigano na kuongeza kuwa wito wa amani na mazungumzo unapaswa kwenda sambamba na usitishaji wa mapigano wa upande mmoja na maono ya suluhu, hii ikiwa ni kulingana na ofisi yake iliyomnukuu wakati akizungumza kwa simu njia ya simu.

Rais Volodymyr Zelenskiy pia atazungumza na rais Erdogan kuhusiana na vita vya nchini mwake.Picha: Ukrainian Presidential Press Service/REUTERS

Rais Erdogan na Putin wamekuwa wakifanya mazungumzo ya mara kwa mara tangu Urusi ilipoivamia Ukraine mapema mwaka jana. Ikumbukwe Uturuki, iliwahi kuandaa duru mbili za mazungumzo ya amani yaliyosidia kufikiwa kwa makubaliano yaliyoungwa mkono na Umoja wa Mataifa ya kurejesha usafirishaji wa nafaka wa Ukraine katika Bahari Nyeusi na hii leo Putin amerudia tena kumwambia Erdogan kwamba kwamba vizuizi vyote vimeondolewa.

Erdogan anatarajiwa kufanya mazungumzo ya muendelezo na rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine, baadaye hii leo. Erdogan amekuwa akitumia fursa ya uhusiano wake mzuri na Moscow na Kyiv kujaribu na kupatanisha mataifa hayo yanayozozana akijaribu kuwakutanisha wakuu hao wawili nchini Uturuki kwa ajili ya mazungumzo ya kilele ya amani.

Rais Vladimir Putin akiwa na kiongozi wa kanisa la Orthodox nchini humo Patriarch KirillPicha: Mikhail Metzel/Sputnik/Kremlin Pool Photo/AP/picture alliance

Kanisa la Orthodox la Urusi laomba kusitishwa mapigano.

Na huko Moscow, mkuu wa Kanisa la Orthodox la Urusi Patriarch Kirill ametoa wito kwa pande zinazohasimiana kwenye vita hivyo kufikia makubaliano ya saa 36 za kusitisha vita wakati ya sherehe za Krismasi ya Orthodox zinazofanyika mwishoni mwa wiki hii, ingawa wito huo ulionekana ni kama hautaweza kubadilisha chochote kuelekea kusitishwa kwa vita hivyo.

Kiongozi huyo, aliomba vita kusimama kuanzia mchana wa Ijumaa hadi usiku wa manane wa Jumamosi, kwa masaa ya Urusi. Kanisa la Orthodox nchini Urusi linatumia kalenda la kizamani ya Julian, na huadhimisha siku ya mwaka mpya kila Januari 7.

Msaidizi mwandamizi wa rais Zelenskiy Mykhailo Podolyank ameufananisha mwito huo wa Kanisa la Orthodox kama mtego usio na maana na sehemu ya propaganda za Urusi. 

Na kutoka huko Oslo, taarifa zinasema, Ujerumani imeahidi kuendelea kuipatia silahaUkraine kwa kuangazia hali ya vita, hii ikiwa ni kulingana na naibu kansela Robert Habeck, anayehudhuria mkutano wa masuala ya uchumi jijini Oslo. Habeck amesema, Berlin haitaacha kuisaidia Ukraine, hata baada ya rais Emmanuel Macron kutangaza kupeleka magari ya kivita nchini humo.

Soma Zaidi: Marekani, Ufaransa zaapa kuiwajibisha Urusi kwa vita Ukraine