PYONGYANG: Korea Kaskazini yakubali kutoa mabaki ya wanajeshi wa Marekani
10 Aprili 2007Gavana wa jimbo la New Mexico nchini Marekani, Bill Richardson, amesema Korea Kaskazini imekubali kupeana mabaki ya wanajeshi sita wa Marekani waliouwawa wakati wa vita vya Korea kati ya mwaka wa 1950 na 1953.
Akiwa ziarani nchini Korea Kaskazini, gavana huyo amesema baada ya kukutana na jenerali wa jeshi la Korea Kaskazini, kwamba uamauzi huo ni kitendo cha ukarimu.
Gavana Richardson atayasafirisha mabaki ya wanajeshi hao nchini Korea Kusini hapo kesho. Baadaye yatasafirishwa hadi kwenye kambi ya jeshi la Marekani huko Hawaii ili kutambuliwa.
Kitengo cha jeshi la Marekani kinachoshughulikia kuwatafuta wanajeshi zaidi ya 8,100 ambao hawajulikani waliko tangu vita vya Korea, kimesema kitatuma wajumbe mara tatu mwaka huu kwenda Korea Kaskazini kutafuta mabaki.
Gavana Bill Richardson amesema amekutana na mjumbe wa Korea Kaskazini katika mzozo wa nyuklia na kumsisitizia kuhusu kukifunga kinu cha nyuklia kwa wakati uliowekwa na kutoa orodha ya shuhguli na nyenzo za nyuklia lakini hakusema jibu alilopewa na afisa huyo.