Pyongyang.China yafanya mazungumzo na kiongozi wa Korea ya Kaskazini.
19 Oktoba 2006Imeripotiwa kuwa China imetuma mjumbe wake ambae amekukutana na Kiongozi wa Korea ya Kaskazini Kim Jong-il, kufuatia kuongezeka kwa wasi wasi juu ya jaribio la nyuklia la Korea ya Kaskazini.
Mjumbe huyo ni waziri wa zamani wa mambo ya kigeni wa China Tang Jiaxuan, inaaminika kwamba amepeleka ujumbe kutoka kwa Rais wa China Hu Jintao aliyetoa mwito wa kuvumiliana.
Mkutano huo umekuja kufuatia maafisa wa Korea ya Kaskazini kudokeza kuwa wanataka kufanya jaribio jengine.
Nae waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani bibi Condoleezza Rice ameionya kuwa hatua zaidi zitachukuliwa ikiwa Korea ya Kaskazini itafanya jaribio jengine.
Bibi Rice yupo nchini Korea ya Kusini katika hatua yake ya pili ya ziara yake barani Asia, ili kutafuta uungwaji mkono katika utekelezaji wa vikwazo ilivyowekewa Korea ya Kaskazini.
Ziara ya bibi Condoleezza Rice itamchukua vile vile hadi China na Urusi hapo kesho.
Wakati huo huo Waziri wa Mambo ya kigeni wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier, akiwasilisha ripoti ya mwaka ya serikali kuu Bungeni hii leo, kuhusu kupunguzwa silaha amesema.
”Kwa mkakati madhubuti wa sera za kupunguza silaha, tunataka kuzuia hatari ya mashindano ya kinyuklia katika sehemu nyengine za dunia na umuhimu wake unakutikana kufuatia jaribio la kinyuklia la Korea ya Kaskazini. Jaribio hilo na uchokozi wa serikali ya Korea ya Kaskazini, ni kinyume na makubaliano ya kutosambaza silaha. Ndio maana tunaunga mkono jibu la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa”.