1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Qatar "inawanyanyasa" wafanyakazi wa ujenzi

18 Novemba 2013

Shirika la Kimataifa la Kutetea Haki za Binaadamu – Amnesty International limeshutumu “kiwango kikubwa cha unyanyasaji wa wafanyakazi wa ujenzi nchini Qatar, kwenye ripoti yake ya hivi punde

Picha: Getty Images

Amnesty Internationa imeitaka Qatar kuitumia fursa ya kuandaa dimba la Kombe la Dunia mwaka wa 2022 kwa kuonyesha kuwa imejitolea kulinda haki za binaadamu. Ripoti ya Amnesty International inasema wafanyakazi wa kigeni wanaishi kama “wanyama“, neno ambalo shirika hilo limesema watafiti wake walimsikia mkurugenzi mmoja wa kampuni ya ujenzi akilitumia kuwaelezea wafanyakazi hao.

Salil Shetty ni Katibu Mkuu wa Amnesty International na anasema "Kitu kimoja ambacho tunaamini kinapaswa kutatuliwa haraka ni mfumo wa kutoa vibali vya kuondoka. Tunadhani hilo linastahili kushughulikiwa haraka. Matatizo ya ukiukaji wa haki za binaadamu kuhusiana na wafanyakazi wa kigeni nchini Qatar ni makubwa mno. Yamesambaa kote. Siyo matukio machache tu".

Makundi ya kutetea haki za binaadamu yanawataka watu wasusie Dimba la Kombe la Dunia nchini QatarPicha: Reuters

Serikali ya Qatar inapinga madai hayo kuwa inawanyanyasa wafanyakazi wa kigeni, ikisema itayaijumuisha ripoti hiyo katika uchunguzi ambao tayari ilianzisha. Nasser al-Khater kutoka kwa kamati ya Kombe la Dunia 2022 nchini Qatar anasema nchi hiyo inajaribu kurekebisha sheria hizo….."ni nchi inayokuwa kwa kasi sana kwa idadi ya watu, na mojawapo ya nchi zinazokuwa kwa kasi kiuchumi ulimwenguni, hivyo ni wazi vitu haviwezi kuimarika kwa wakati mmoja."

Ripoti hiyo imetoa wito kwa Shirikisho la Soka Ulimwenguni FIFA kulishinikiza taifa hilo la Guba kuimarisha mazingira ya wafanyakazi wa kigeni, wengi wao ambao wanatokea Kusini au Kusini mashariki mwa Asia.

Wafanyakazi hao wanalalamika kutolipwa mishahara yao, mazingira magumu na hatari ya kufanyia kazi, na viwango vya kushutusha vya malazi. Wengi wao wamekwama nchini Qatar wasiweze kuondoka. Wafanyakazi wengi pia wameripoti hali mbaya ya afya na viwango duni vya usalama.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/Reuters

Mhariri:Yusuf Saumu