1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Qatar kuchukuliwa hatua zaidi na mataifa ya Ghuba

7 Julai 2017

Nchi nne za Kiarabu zinazoitenga Qatar ziliapa siku ya Ijumaa kuchukua hatua zaidi dhidi ya taifa hilo la Ghuba lenye utajiri wa mafuta.

Ägypten Außenminister Treffen in Kairo
Picha: Reuters/K. Elfiqi

Hii ni baada ya Qatar kukataa kuyakubali masharti yake kufuatia madai kwamba taifa hilo linaunga mkono masuala ya itikadi kali. Huku hayo yakiarifiwa, Marekani imesema ina wasiwasi kwamba huenda mzozo huo wa mataifa hayo ya Ghuba ukaendelea kwa wiki au miezi kadhaa.

Saudi Arabia, Falme za Kiarabu, Misri na Bahrain katika taarifa ya pamoja iliyopeperushwa katika vyombo vya habari vya Ghuba Alhamis, ziliishutumu Qatar kwa kulemaza juhudi zote za kuupatia ufumbuzi mzozo huo na kwamba inalenga kuendeleza sera yake ambayo inahujumu usalama wa kanda hiyo. Wameapa kuchukua hatua zote za kisiasa, kiuchumi na kisheria dhidi ya Qatar. Hawakuweka wazi ni hatua zipi watakazozichukua ingawa hapo awali maafisa walisema wanapendekeza kuongeza juhudi za kuitenga Qatar kiuchumi.

Wizara ya mambo ya nje ya Marekani ilisema Waziri wa mashauri ya kigeni Rex Tillerson atasafiri katika kanda hiyo kujaribu kutafuta suluhu la mzozo huo na anatarajiwa kuzuru Kuwait Jumatatu, baada ya Kuwait kumpatia mwaliko rasmi ili kuujadili mzozo huo.

Idara ya ujasusi ya Ujerumani itaiondolea Qatar lawama ya kuunga mkono ugaidi

Msemaji wa wizara hiyo Heather Nauert alisema wasiwasi wa Marekani kuhusiana na mzozo huo unazidi kuongezeka.

"Bado tuna wasiwasi kuhusiana na hali inayoendelea kati ya Qatar na nchi wanachama wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba," alisema Heather. "Wasiwasi wetu umeongezeka zaidi kwa sasa kwamba mzozo huo umegonga mwamba kwa sasa. Tunaamini kwamba kuendelea huku kunaweza kuendelea kwa wiki au hata miezi zaidi. Huenda hata mzozo huu ukazidi."

Viongozi wa mataifa ya Ghuba wakiujadili mzozo wao na QatarPicha: Getty Images/AFP/K. Elfiqi

Wakati huo huo, Ujerumani imesema idara yake ya ujasusi itahusika katika kuiondolea Qatar lawama ya madai ya kuyaunga mkono makundi ya kigaidi. Waziri wake wa mambo ya nje Sigmar Gabriel aliizuru Saudi Arabia, Qatar na Kuwait ambayo ndiyo mpatanishi katika mzozo huo.

Nchi hizo nne za Kiarabu zilikata uhusiano na kusitisha mawasiliano yake ya ndege, ardhini na hata majini na Qatar mapema mwezi uliopita. Baadaye walitoa orodha ya matakwa 13 kwa Qatar, yakiwemo kusitisha uhusiano wake na makundi ya kigaidi, kusitisha uhusiano wake na Iran na kufunga vyombo vya habari likiwemo shirika la habari la Al Jazeera.

Nchi zinazoipinga Qatar zinasema Qatar haina nia ya kuusuluhisha mzozo

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amesema masharti hayo dhidi ya Qatar hayakubaliki.

Rais wa Uturuki Reccep Tayyip Erdogan anapinga vikwazo dhidi ya QatarPicha: Reuters/M. Sezer

"Haya masharti 13 kimsingi ni ya kuifanya nchi ipoteze uhuru wake," alisema Erdogan. "Qatar ni taifa na hili halikubaliki katika hali yoyote ile."

Qatar ilitoa jawabu lake baada ya masharti hayo dhidi yake kupitia barua iliyoandikwa na Emir wa nchi hiyo Tamim bin Hamad Al Thani, barua iliyowasilishwa kwa Kuwait ingawa yaliyomo katika barua hiyo hayajawekwa wazi.

Lakini nchi hizo zinazoipinga Qatar zimesema kwamba yaliyomo kwenye barua hiyo sio mazuri na hayazingatii uzito wa mzozo huo. Qatar imekataa katakata kwamba inaunga mkono makundi ya kigaidi na imekataa pia kulifunga shirika lake la habari la Al Jazeera na inasema uhuru wake unakiukwa.

Mwandishi: Jacob Safari/APE/AFPE

Mhariri: Josephat Charo