1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya kuongeza muda wa kusitisha vita Gaza yaendelea

Angela Mdungu
30 Novemba 2023

Misri na Qatar zimesema zinaendelea kufanya mazungumzo yanayolenga kuongeza muda wa kusitisha vita katika ukanda wa Gaza kati ya Israel na kundi la Hamas kwa siku mbili zaidi.

Mzozo wa Mashariki ya Kati | Usitishaji mapigano Ukanda wa Gaza
Mkaazi wa Gaza akitazama madhara yaliyotokana na mashambulizi ya anga mjini Khan Yunis, GazaPicha: Ahmad Hasaballah//Getty Images

Mkuu wa idara ya habari ya Misri Diaa Rashwan amesema kurefushwa kwa muda wa usitishaji wa mapigano kwa siku mbili zaidi ni juhudi zinazofanywa ili kuwawezesha wafungwa wengi zaidi na mateka kuachiliwa huru na kuingiza misaada mingi zaidi ya kiutu katika Ukanda wa Gaza.

Soma zaidi: UN: Kuundwe mataifa mawili katika mzozo wa Israel-Hamas

Wakati mazungumzo hayo ya kuongeza muda zaidi wa kusimamisha vita yakiendelea, shirika la hilali nyekundu la Palestina  limesema kuwa malori 1,132 yaliyobeba misaada ya kiutu kwa ajili ya Ukanda wa Gaza yameingia katika ukanda huo kupitia mpaka wa Rafa tangu mapigano yaliposimamishwa kwa muda.

Blinken apongeza kuongeza muda wa usitishwaji vita

Katika hatua nyingine, waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani  Antony Blinken amesema kuwa makubaliano ya usitishwaji vita kati ya Israel na kundi la Hamas yanaonesha matokeo na yanapaswa kuendelea.

Blinken ameyasema hayo mjini Tel Aviv wakati alipokutana na rais wa Rais Isaac Herzog.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Antony Blinken na Rais wa Israel Isaac HerzogPicha: Saul Loeb/Pool Photo/AP Photo/picture alliance

Blinken alikutana pia na kufanya mazungumzo na waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu aliyesisitiza kuwa wataendeleza vita hadi malengo ya kuachiliwa mateka, kuliangamiza kundi la Hamas na kuhakikisha kwamba Gaza haitakabiliwa na kitisho kama hicho yatakapotimia.

Katika ziara yake ya tatu tangu mzozo kati ya Israel na hamas ulipoanza, Blinken anatarajiwa pia kukutana na rais wa mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas.

Kwingineko Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Annalena Baerbock amepongeza hatua ya kurefushwa kwa muda wa usitishaji wa vita katika ukanda wa Gaza. Baerbock amesema amani kwa Waisrael na Wapalestina inategemea kupatikana kwa suluhisho la pamoja la kuhakikisha kunakuwa na usalama katika pande hizo mbili.