Qatar na Uturuki kushiriki mazungumzo ya Gaza
8 Oktoba 2025
Mazungumzo haya yasiyo ya moja kwa moja kati ya Israel na Hamas yanafanyika katika mji wa mapumziko wa Sharm El-Sheikh, yakiongozwa na mpango wa vipengele 20 uliopendekezwa na Rais wa Marekani Donald Trump mwezi uliopita.
Mapema jana Rais Trump aliwaambia waandishi wa habari akiwa Ikulu ya White House kwamba kuna uwezekano halisi kwamba wanaweza kufanikisha hatua fulani na kuongeza kuwa wajumbe wa Marekani pia wanashiriki katika mazungumzo hayo.
Hamas inataka dhamana ya kusimamia makubaliano
Nchini Misri ambako mkutano huo unaendelea Mwakilishi mkuu wa Hamas, Khalil El-Hayya, amesema kundi hilo la Kiislamu linataka "dhamana kutoka kwa Rais Trump na nchi zinazodhamini mazungumzo kwamba vita vitamalizika kabisa, kauli ambayo imejibiwa na Trump akisema, "Naam, dhamana ya msingi ni kwamba mara tu makubaliano haya yatakapofikiwa, kama yatafikiwa, zingatia mazungumzo bado yanaendelea. Tutafanya kila liwezekanalo. Tuna nguvu kubwa, na tutafanya kila tuwezalo kuhakikisha kila mtu anazingatia makubaliano hayo."
Mazungumzo haya yanafanyika wakati Israel ikiadhimisha kumbukumbu ya miaka miwili tangu shambulio la Hamas la Oktoba 7 ambalo ndilo lililosababisha kuanza kwa vita hivi. Shambulio hilo liliua watu 1,219, wengi wao wakiwa raia, kwa mujibu wa takwimu za AFP zilizotokana na vyanzo rasmi vya Israel. Wapiganaji pia waliwateka watu 251 na kuwapeleka Gaza, ambapo 47 bado wanashikiliwa mateka, wakiwemo 25 ambao jeshi la Israel linasema wamefariki dunia.
Kuongezeka kwa shinikizo la kumalizwa vita vya Gaza
Shinikizo la kimataifa la kumaliza vita limeongezeka, huku sehemu kubwa ya Gaza ikiwa imeharibiwa, njaa ikitangazwa na Umoja wa Mataifa, na familia za mateka wa Kiyahudi zikiendelea kutamani wapendwa wao warejeshwe nyumbani.
Ripoti ya uchunguzi wa Umoja wa Mataifa mwezi uliopita ilishutumu Israel kwa kutekeleza mauaji ya kimbari Gaza, huku mashirika ya haki za binadamu yakishutumu Hamas kwa uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu wakati wa shambulio la Oktoba 7. Pande zote mbili zimekanusha tuhuma hizo.