Qatar yaitisha mkutano kulaani "uchokozi" wa Israel
15 Septemba 2025
Duru kutoka vyanzo vya kidiplomasia zinaarifu kwamba viongozi hao wanalenga kuweka kando tofauti zao na kuchukua msimamo wa pamoja wa kuikosoa Israel na kuonesha mshikamano na Qatar kama walivyofanya baada ya kutokea mashambulizi ya Israel kwenye mji mkuu, Doha.
Rasimu ya azimio la mkutano huo ambayo shirika la habari la Reuters imeiona, inaonesha viongozi hao watatoa hadhari kwamba mashambulizi ya Israel nchini Qatar ya wiki iliyopita na "matendo yake mengine ya kichokozi yanahatarisha jitihada za mapatano na azma ya kuishi pamoja kwa amani kwenye kanda hiyo."
Mashambulizi hayo ambayo Israel inasema yalikuwa halali kwa sababu yaliwalenga viongozi wa kundi la Hamas, yamezusha hasira na ukosoaji mkubwa kimataifa na kuteteresha mahusiano kati ya Israel na majirani zake wa kiarabu.
Tangu yalipotokea, viongozi wa kanda hiyo na wale wa mataifa ya kiislamu wameonesha umoja kwa kutoa rai ya kuwekwa mbinyo zaidi dhidi ya Israel ambayo tayari inaandamwa na shinikizo la kumaliza vita vya Ukanda wa Gaza.
Qatar yataka jumuiya ya kimataifa "isifumbie macho matendo ya Israel"
Katika mkutano wa ngazi ya mawaziri uliofanyika siku ya Jumapili kuelekea mkutano wa leo Jumatatu, Waziri Mkuu wa Qatar ambaye pia ni waziri wa mambo ya nchi za nje, Sheikh Mohammed bin Abdulrahman Al Thani amesema jumuiya ya kimataifa ni sharti iiwajibishe Israel kwa matendo yake aloyaita "ya uhalifu."
"Ni wakati sasa kwa jumuiya ya kimataifa kuacha tabia ya undumilakuwili na iiwajibishe Israel kwa uhalifu iloufanya. Hatupaswi kukaa kimya mbele ya mashambulizi haya ya kihayawani na itafaa tuchukue hatua za uhakika na zenye mashiko kuzuia mashambulizi mengine, ambayo kama tukiyanyamazia hayatakoma. Na vyovyote tutakavyofanya, tutajikuta, tunabakia katika mfululizo wa matukio ya umwagaji damu na uharibifu na hakuna atakayobaki salama mbele ya hatari hii na taathira zake. ", amesema Sheikh Al Thani.
Miongoni mwa viongozi wanaotazamiwa kuhudhuria mkutano wa leo ni pamoja na Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki, Masoud Pezeshkian wa Iran na Waziri Mkuu wa Iraq Mohammed Shia al-Sudani.
Kiongozi wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina, Mahmoud Abbas, tayari amewasili Doha tangu jana Jumapili kushiriki mkutano huo.
Rubio ziarani Israel katikati ya mbinyo unaoukabili utawala mjini Tel Aviv
Katika hatua nyingine, Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani, Marco Rubio, yuko nchini Israel tangu jana kwa ziara inayolenga kutafuta majibu kuhusu hatma ya mzozo wa Gaza hasa katika wakati jitihada za upatanishaji zimeingia kiwingu.
Rubio amesema Washington inataka kuzungumza kuhusu mateka wanaoshikiliwa Gaza pamoja na hatua za kuujenga upya ukanda huo.
Shambulizi la Israel nchini Qatar, taifa ambalo limeongoza jitihada za upatanishi tangu kuanza kwa vita, limezidisha mashaka kuhusu uwezekano wa kupatikana makubaliano yoyote ya kusitisha vita Ukanda wa Gaza.
Ziara ya Rubio inazingatiwa kuwa na lengo la kuonesha mshikamano na Israel katikati ya lawama ya kimataifa kwa mashambulizi yake mjini Doha.
Vilevile mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa unaendelea mjini New York unatarajiwa kuhodhiwa na mjadala kuhusu uundwaji taifa la Palestina na kutambuliwa ka dola hiyo na mataifa kadhaa ya magharibi, hali ambayo huenda itaetenga zaidi Israel kimataifa.