1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Qatar yajiondowa upatanishi vita vya Gaza

9 Novemba 2024

Qatar imejiondowa kwenye upatanishi wa kusaka makubaliano ya kusitisha vita vya Gaza na kuachiliwa kwa mateka na imelionya kundi la Hamas kwamba ofisi yake ya Doha haifanyi tena kazi iliyokusudiwa.

Qatar | Amir wa Qatar | Tamim bin Hamad Al Thani
Amir Tamin bin Hamad Al Thani wa Qatar.Picha: Jacquelyn Martin/AP Photo/picture alliance

Chanzo kimoja cha kidiplomasia kimeliambia shirika la habari la AFP siku ya Jumamosi (Novemba 9) kwamba tayari Qatar ilishazijulisha Israel na Hamas kwamba madhali zinakataa kufikia makubaliano kwa nia njema, basi taifa hilo la Ghuba lisingeweza kuendelea kuwa mpatanishi. 

Kwa mujibu wa chanzo hicho, ambacho hakikutaka kutajwa jina, ofisi ya Hamas mjini Doha iliarifiwa kuwa "imepoteza uhalali wa kuwapo kwake, kwa kuwa haifanyi kazi iliyokusudiwa."

Soma zaidi: 

Maafisa wa Hamas mjini Doha walisema hawakuwa wamepokea amri ya kuondoka kutoka serikalini.

Qatar pamoja na Marekani na Misri zimekuwa kwa miezi kadhaa zikijihusisha na mikutano ya upatanishi ambayo imeshindwa kuzaa matunda.

Tayari Qatar ilishawajulisha wapatanishi wenzake juu ya uamuzi wake huo, ikisema kwamba itakuwa tayari kurejea kwenye jukumu hilo pale Israel na Hamas zitakapokubali kupatanishwa.