1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroIsrael

Majadiliano zaidi yanahitajika kuhusu mpango wa amani

1 Oktoba 2025

Msuluhishi mkuu wa mzozo wa Israel na Hamas Qatar imesema kunahitajika mazungumzo zaidi kuhusu mpango wa amani wa Rais Donald Trump wa kumaliza vita kwenye Ukanda wa Gaza, wakati Hamas ikiangazia namna ya kuujibu.

Qatar| Mkutano maalum wa kilele wa Umoja wa Nchi za Kiarabu baada ya mashambulizi ya anga ya Israel | Saoud bin Abdulrahman al-Thani | Mansour bin Zayed Al Nahyan
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Masuala ya Ulinzi wa Qatar Sheikh Saoud bin Abdulrahman al-Thani akimpokea Makamu wa Rais wa UAE na Naibu Waziri Mkuu Sheikh Mansour bin Zayed Al Nahyan kabla ya mkutano wa dharura wa kilele wa Waarabu na Kiislamu, kujadili shambulio la Israel dhidi ya Hamas katika ardhi ya nchi hiyo ya Ghuba, mjini Doha, Qatar Septemba 15, 2025.Picha: Qatar News Agency/REUTERS

Matamshi hayo ya Qatar yanaakisi kile kinachoonekana kama Mataifa ya Kiarabu kutoridhishwa na waraka wa mpango huo wenye vipengele 20 uliotangazwa siku ya Jumatatu na Rais Donald Trump sambamba na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu aliyesema anauunga mkono. Umoja wa mataifa nao umeseama licha ya kwamba hawakushirikishwa kwenye maandalizi uko tayari kuongeza misaada inayopelekwa Gaza mara tu mazingira yatakaporuhusu.

Maafisa wa mataifa matatu ya Kiarabu waliliambia shirika la habari la AFP kwamba pendekezo la awali lililofanyiwa kazi kwa ushirika wa mataifa hayo na yale ya Kiislamu pamoja na Trump limefanyiwa mabadiliko na kuipendelea zaidi Israel. Maafisa hao waliotoka kwenye mataifa yenye nguvu ya kikanda na waliohusika kwenye mazungumzo hayo lakini hawakutaka kutambulishwa.

Bado haiko wazi ni kwa ukubwa gani Mataifa ya Kiarabu hayajaridhika na yameendelea kueleza kuunga mkono kwa kiasi kikubwa mpango huo. Lakini matamshi haya ya Qatar yanaashiria kutahitajika majadiliano zaidi juu ya baadhi ya vipengele licha ya Rais Trump kuwapa Hamas siku tatu hadi nne kutoa majibu.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Johann Wadephul akizungumza nje ya Mkutano wa Baraza kuu la Umoja wa Mataifa, New York Septemba 26, 2025Picha: Kay Nietfeld/dpa/picture alliance

Mjini Berlin, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Johann Wadephul amesema wako tayari kusaidia utekelezwaji wa mpango huo ingawa anadhani haitakuwa rahsi kuanza kutekelezwa mara moja. Alipozungumza na shirika la habari la Funke amesema bado kuna maswali magumu mengi kuhusu namna utakavyofanya kazi, hakikisho la usalama, namna misaada ya kiutu itakavyorejeshwa pamoja na uratibu wa ujenzi mpya wa Gaza. Akasema huo ni mchakato mgumu.

Mpango wa amani wa Gaza ni 'uingiliaji wa kigeni,' 

Katika hatua nyingine, mkurugenzi mwenza wa Taasisi ya Palestine Institute for Public Diplomacy, PIPD Ines Abdel Razek, alipozungumza na DW kuhusiana na mpango huo amesema anadhani watu wanatakiwa kutambua kwamba sio mpango wa Wapalestina na kwa maana hiyo hawana fursa ya kufanya maamuzi yao. Akasema huo ni ukiukwaji mkubwa wa haki yao ya  kujitawala na kujiamulia wenyewe.

Amesema na badala yake utaweka mazingira mazuri zaidi ya uwezekano wa jeshi la Israel kukalia kwa mabavu na hatimaye kulinyakua eneo la Gaza na kuongeza kuwa huo ni ukoloni mtupu na uingiliaji wa kigeni huko Gaza wa watu ambao wanahusika na mateso ya watu wa Palestina.

Tunisia, Tunis: Meli za Msafara wa Kimataifa wa Sumud Flotilla zikiwa njiani kuelekea Gaza zikiwa zimetia nanga kwenye pwani ya Sidi Bou Saïd huko Tunis, Septemba 9, 2025Picha: Str/AP Photo/dpa/picture alliance

Italia yawatahadharisha Sumud Flotilla

Mbali na hayo, Italia imewatahadharisha waratibu msafara wa Sumud Flotilla unaopeleka misaada Gaza kwamba huenda Israel ikaichukulia hatua hiyo kama "kitendo cha uchokozi." Waziri wa Ulinzi wa Italia alitangaza kwamba meli ya kijeshi iliyopelekwa kwenye eneo hilo itakuwa tayari kumchukua mshiriki yoyote atakayetaka kuachana na msafara huo na tahadhari ya mwisho itatolewa leo, Oktoba Mosi.

Msafara huo wa boti zipatazo 40 za kiraia unaelekea Gaza ukiwa umebeba wabunge, wanasheria na wanaharakati ikiwa ni pamoja na mwanakaratati wa mazingira Gretha Thunberg na tayari Waziri Mkuu wa Italia Giorgia Meloni aliwaonya kusitisha mara moja msafara huo.

Msafara huo umearifu mapema leo kwamba visa vya droni dhidi yao vinaongezeka na hasa baada ya kuingia kwenye eneo hatari zaidi ambako wenzao walishambuliwa hapo kabla.

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW