QUITO : Ecuador yagoma kumuachilia Rais aondoke nchini
23 Aprili 2005Rais wa Ecuador aliyen’golewa madarakani Lucio Gutierrez ameendelea kujichimbia kwenye ubalozi wa Brazil wakati Umoja wa Mataifa ya Amerika ukijadili uhalali wa kuondolewa kwake madarakani.
Serikali mpya ya Ecuador na maafisa wa serikali ya Brazil bado wako katika mazungumzo juu ya ama au ala kumruhusu Guiterrez kuondoka bila ya matatizo kwenda Brazil alikopatiwa hifadhi ya kisiasa baada ya bunge la nchi hiyo kupiga kura ya kumuondowa kwenye wadhifa huo wa Urais.
Umati wa watu umeufunga uwanja wa ndege kumzuwiya Guiterrez kukimbia nchi hiyo baada ya kuangushwa hapo Jumatano.
Nafasi yake inachukuliwa na Makamo wake wa Rais Alfredo Palacio ambaye anatarajiwa kutumikia kipindi kilichobakia cha Guiterrez cha miaka minne kinachomalizika mapema mwaka 2007. Guiterrez ameondolewa madarakani kufuatia miezi kadhaa ya maandamano dhidi ya majaribio yake ya kuwatimuwa mahakimu wa mahkama kuu wanaopendelea upinzani.
Rais huyo anakuwa kiongozi wa tatu kun’golewa nchini humo katika kipindi cha miaka minane.