1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rabsha kwenye mkutano kati ya Merkel na al-Sisi

Admin.WagnerD4 Juni 2015

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ameikosoa Misri kwa kuitumia adhabu ya kifo, lakini wakati huo huo ameahidi kuimarisha uhusiano na nchi hiyo katika sekta ya uchumi na vita dhidi ya kuenea kwa itikadi kali ya Kiislamu.

Kansela Angela Merkel na mgeni wake, rais Abdel Fatah al-Sisi mjini Berlin
Kansela Angela Merkel na mgeni wake, rais Abdel Fatah al-Sisi mjini BerlinPicha: Reuters/F. Bensch

Hayo yamejiri wakati wa ziara ya rais wa Misri Abdel Fatah al-Sisi iliyotajwa kuwa yenye utata katika mji mkuu wa Ujerumani, Berlin, jana Jumatano. Rais al-Sisi wa Misri alipokelewa kwa gwaride la kijeshi aliloandaliwa na serikali, pamoja na maandamano mitaani yaliyotayarishwa na wapinzani wa sera zake.

Vyombo vya habari vya Ujerumani viliipinga ziara hiyo, kwa sababu rais al-Sisi anaunga mkono serikali za kiarabu zinazotumia ukandamizaji kupambana na itikadi kali za kiislamu.

Katika mkutano wa pamoja na waandishi wa habari baada ya mazungumzo, Bi Merkel alitetea msimamo wa serikali yake.

''Kwanza napenda kusema kwamba uhusiano na Misri ni muhimu na ni wa kimkakati'' alisema Merkel, na kuongeza kuwa Misri ni nchi kubwa katika eneo la Mashariki ya Kati ambayo utengamano wake umeyumba, na Ujerumani inataka kuiona nchi hiyo ikiwa na uchumi imara, ili iweze kuwapa matumaini watu wake ambao wengi ni vijana. Bi Merkel hali kadhalika alisema mazungumzo baina yake na rais al-Sisi yalijikita juu ya ushirikiano wa kiuchumi.

Sera za al-Sisi zamgeuka

Rais Abdel Fatah al-Sisi Julai mwaka 2013 alimuondoa madarakani rais Mohamed Mursi anayetoka katika Udugu wa Kiislamu, na alianzisha ukandamizaji mkubwa dhidi ya makundi yaliyomuunga mkono rais huyo kutoka Udugu wa Kiislamu na makundi mengine ya wanaharakati yasio ya kidini.

Mwanamke mmoja alimuita rais al-Sisi ''muuaji'' wakati wa mkutano na waandishi wa habariPicha: Reuters/F. Bensch

Ukandamizaji huo uliwauwa mamia ya wafuasi wa Mohamed Mursi na kuwaweka maelfu gerezani, na wengine wengi wamehukumiwa adhabu ya kifo katika kesi za halaiki na za muda mfupi, akiwemo Mursi mwenyewe.

Kansela Merkel amesema daima anapinga adhabu ya kifo, na kwamba hakuna sababu hatia yoyote, hata ile yenye uhusiano na ugaidi, inaweza kuhalalisha adhabu hiyo.

Katika maelezo yeke mbele ya waandishi wa habari, rais al-Sisi alitaka kutuliza wasiwasi wa wale wanaozipinga sera zake.

''Tumezungumza kuhusu demokrasia, na ningependa kutumia fursa hii kusema kwamba hata sisi tunapenda demokrasia na uhuru pamoja na maadili ya kidemokrasia. Lakini tunaishi katika wakati mgumu na bila shaka tuna mapungufu. Pengine hatufanikiwi kufikisha ujumbe wetu kwa Ulaya, hii ni fursa ya fursa ya kufanya hivyo''. Alisema rais huyo wa Misri.

Sauti za ukosoaji na uungaji mkono

Katika mkutano huo wa pamoja kati ya Kansela Merkel na rais al-Sisi, mwanamke mmoja aliingilia kati, na kupaza sauti akimuita rais huyo ''muuaji''. Waandishi wengi wa habari wa Misri walimuunga mkono rais wao kusema, ''idumu Misri'', wakati Kansela Merkel na mgeni wake walipokuwa wakiondoka kwenye chumba cha mkutano.

Walikuwepo pia walioandamana kumuunga mkono rais al-SisiPicha: Reuters/F. Bensch

Wakati wa ziara hiyo ya siku mbili rais al-Sisi alikutana pia na rais wa Ujerumani Joachim Gauck, lakini alisusiwa na spika wa bunge Norbert Lammert, aliyemshutumu kukanyaga upinzani.

Vyombo vya habari vya Misri vimeripoti kuwa rais al-Sisi alitarajiwa kusaini makubaliano kadhaa na makampuni ya Ujerumani, katika sekta za nishati endeleve na mafuta.

Mwandishi:Daniel Gakuba/afpe, dpae

Mhariri:Iddi Ssessanga

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi